Hapa na Pale
Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) limeripoti shukrani zake baada ya kupokea msaada wa dola milioni 6 kutoka Saudi Arabia, kutumiwa kufadhilia chakula watu wa Ghaza. Kadhalika, Kampeni ya Watunzaji wa Msikiti Miwili Mitukufu kwa Faraja ya Umma wa Ghaza ya Saudi Arabia imeipatia UNRWA mchango ziada wa dola 500,000 zitakazotumiwa kulipia nishati ya kuwasaidia wenyeji kujihifadhi na majira ya baridi kwenye eneo la uhasama; na pia kutumiwa kupampu maji na kuunguzia takataka, kadhia ambazo ni muhimu katika kuzuia miripuko ya maradhi ya kuambukiza. Fedha zilizofadhiliwa chakula zitaiwezesha UNRWA kuwapatia watu 500,000 wa Ghaza vifurushi vya vyakula vya kutumiwa kwa siku 60.
Mnamo mwisho wa wiki iliopita, Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) amesema kuwa watafadhilia msaada wa dola milioni 5 kutumiwa kwenye sekta ya afya Zimbabwe, ili kupamabana na miripuko ya maradhi ya kipindupindu nchini na kudhibiti bora huduma za kijamii ambazo zimeanza kuporomoka. Veneman aliyasema hayo alipokuwa anazuru Zimbabwe, ambapo alionana na Raisi Robert Mugabe pamoja na wadau wengine muhimu nchini, ambao alishauriana nawo pia juu ya taratibu za kuchukuliwa kidharura ili kukidhi mahtiaji ya waathiriwa wa kike na watoto. Kwa mujibu wa takwimu mpya za WHO watu 44,000 walisajiliwa kuambukizwa na kipindupindu nchini Zimbabwe, na kusababisha vifo vya wagonjwa 2,300.
Ripoti mpya ya KM kuhusu hali katika ukanda wa Afrika Magharibi imeripoti kupatikana maendeleo ya kutia moyo, kwenye zile juhudi za kuimarisha usalama na amani katika eneo. Ripoti inasema Ofisi ya UM juu ya Afrika Magharibi (UNOWA) itaendelea kusimamia shughuli za upatanishi kuhusu mizozo ya eneo hilo, ikijumlisha ufuatiliaji juu ya namna mapatano ya Nigeria na Cameroon yanavyotekelezwa kuhusu mzozo wa mipakani katika RasBakaasi. Ofisi ya UNOWA inatilia mkazo zaidi ujenzi wa amani kijumla na kuzuia mizozo isifumke.