KM aihimiza Israel kuondosha vikosi Ghaza na kunasiihi WaFalastina kukomesha hujuma za makombora ya kienyeji
KM Ban Ki-moon alibainisha matumaini yake Ijumapili ya kuwa usmamishaji wa upande mmoja wa mashambulizi ya Israel, ya siku 22 dhidi ya eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza humaanisha matumaini mema kwenye juhudi za kudumisha amani kieneo.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Uchumi wa Mataifa ya Kiarabu, uliofanyika Ijumatatu kwenye mji mkuu wa Kuwait, KM alieleza kuingiwa huzuni kubwa, ikichanganyika na faraja kuhusu hali, kijumla, katika Ghaza. Alisema amehuzunishwa na vifo vya maelfu ya raia na maelfu ya watu waliojeruhiwa, kutokana na mashambulizi yaliofanyika Ghaza katika siku 22 zilizopita. Alisema alipata faraja baada ya Israel kutangaza Ijumapili kuwa inasimamisha mashambulizi Ghaza, na kufuatiwa na ilani ya kundi la WaFalastina la Hamas iliotangaza kusitisha, kwa muda, mapigano. KM aliahidi kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha hatua za haraka zitachukuliwa na jumuiya ya kimataifa, ili kuufadhilia umma muhitaji wa KiFalastina, kwenye Tarafa ya Ghaza, misaada ya kiutu ya kunusuru maisha.