Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM azuru Ghaza na kupendekeza kufanyike uchunguzi juu ya mashambulio dhidi ya UM

KM azuru Ghaza na kupendekeza kufanyike uchunguzi juu ya mashambulio dhidi ya UM

KM wa UM Ban Ki-moon, alikutana leo kwenye mji wa Jerusalem, na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na kumwelezea faraja aliyopata baada ya kutangazwa ilani ya upande mmoja ya kusitisha mapigano.

Alipokuwa Ghaza KM alizuru majengo ya Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA), majengo ambayo wiki iliopita yalishambuliwa mabomu na makombora na vikosi vya Israel. Baada ya ziara hiyo, KM alikutana na waandishi habari na aliwaambia “alishtushwa sana” na athari alizozishuhudia za mashambulio ya majengo ya UM, na hujumu zilizofanywa dhidi ya wafanyakazi wake. Alinasihi kwamba “mashambulio yoyote dhidi ya UM, au watumishi wake, ni vitendo visiokubalika, katu, kimaadili na kisheria na ni mambo ya kuchukiza kabisa.” Alisisitiza kwamba amependekeza kuendelezwe na tumu huru, uchunguzi kamili wa kuwatambua ni nani waliohusika na mashambulizi hayo dhidiya UM, na baadaye kuhakikisha watuhumiwa husika watakaopatikana na hatia watafikishwa mahakamani kukabili mashtaka. Kadhalika, alisema Alkhamisi ijayo atatuma Ghaza tume ya maofisa wa ngazi za juu wa UM, itakayoongozwa na Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani katika Mashariki ya Kati, Robert Serry, pamoja na John Holmes, Mratibu wa UM kuhusu Misaada ya Dharura, kwa lengo la kutathminia mahitaji ya kiutu kwa umma wa Tarafa ya Ghaza.

KM alipokutana na Waziri Mkuu wa Israel Olmert alimweleza ya kuwa Umoja wa Mataifa (UM) utaendelea kuhudumia misaada ya kiutu kwa waathirika wa Ghaza, kwa kima kikubwa kabisa, na vile vile UM utajihusisha kikamilifu kwenye kadhia ya kufufua miradi ya maendeleo ya kiuchumi na jamii kwa masilahi ya wenyeji wa Ghaza.

Baada ya ziara ya Ghaza KM alitembelea mji wa Sderot uliopo Israel kusini. KM alinakiliwa akisema Waisraili na WaFalastina hawatofanikiwa kushuhudia mwisho halisi wa vurugu na mgogoro wao, na wala kupata usalama hakika kwenye maeneo yao mpaka itakapopatikana suluhu ya jumla, kutoka lile fukuto la mvutano baina ya Waisraili na Waarabu, ikijumlisha suluhu ya kuanzisha Taifa Hurru la KiFalastina, jirani na Taifa la Israel, na kuishi pamoja kwa usalama na amani.