Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumanne KM ameripotiwa kutuma risala maalumu ya pongezi kwa kutawazwa kwa Barack Obama kuwa Raisi wa 44 wa Marekani. Risala hiyo ilisema KM ana “matarajio makubwa” kuhusu Uraisi wa Barack Obama kwenye zile juhudi za kutafuta suluhu ya mizozo kadha wa kadha ya ulimwengu iliokabili jumuiya ya mataifa: kama wasiwasi wa kiuchumi; athari za mabadiliko ya hali ya hewa; masuala magumu yanayohusu usalama na amani, ikijumlisha ukomeshaji wa uenezaji wa silaha za kinyuklia na upunguzaji wa silaha; pamoja na mchanganyiko wa matatizo yanayohusu mifumko ya bei za chakula na nishati na vile vile kupwelewa kwa huduma za maendeleo. KM alisema Raisi Obama ameahidi serikali yake ipo tayari kukabiliana na masuala haya bila shaka yoyote!~

Mapema wiki hii mjini Addis Ababa wawakilishi wa UM, Umoja wa Afrika na Serikali ya Sudan walikutana kuzingatia tartaibu za kuchukuliwa kidharura ili kuharakisha kupeleka vikosi vya UNAMID Darfur na kukamilisha, kwa wakati ile jumla inayotakikana kuimarisha amani ya wanajeshi 26,000 pamoja na askari polisi. Serikali ya Sudan ilitia sahihi taarifa ya maelewano na UNAMID itakayohakikisha majeshi ya kimataifa yatapatiwa kila msaada unaohitajika kutekeleza majukumu yao, hususan katika matumizi ya viwanja vya ndege vya Sudan ili kurahisisha upokeaji na usafirishaji wa vifaa vya UNAMID bila matatizo.

Shirika la UM la UNAMIL linalosimamia ulinzi wa amani katika Liberia, limepongeza kuhitimu kwa idadi kubwa ya wanawake kutoka Chuo cha Taifa cha Mafunzo ya Polisi ambapo wanawake 100 kati ya makuruta 150 walifanikiwa kumaliza masomo ya mwaka mmoja, yalioendeshwa na UM. Hivi sasa wanawake wanawakilisha asilimia 13 ya maofisa 3,800 wa Polisi wa Taifa wapya katika Liberia.