Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya Rwanda vyaruhusiwa na serikali ya JKK kuwasaka waasi wa FDLR

Vikosi vya Rwanda vyaruhusiwa na serikali ya JKK kuwasaka waasi wa FDLR

Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) limetangaza rasmi kwamba wanajeshi karibu 2,000 wa Rwanda Ijumanne waliruhusiwa kuingia katika JKK, kwa kupitia eneo la mashariki, kuwasaka waasi wa Rwanda, wa kundi la FDLR, wenye asili ya kiHutu ambao inaripotiwa ndio miongoni mwa makundi yenye kupalilia hali ya wasiwasi kieneo kwa muda wa zaidi ya miaka kumi.

Shirika la MONUC limewasilisha ripoti kwa waandishi habari, inayosisitiza kidhahiri kwamba haihusikani kamwe na operesheni za kijeshi zinazoendeshwa sasa hivi nchini dhidi ya majeshi ya mgambo ya WaHutu waliotokea Rwanda. MONUC ilisema operesheni hizo zinaongozwa na majeshi ya JKK na Rwanda, kutokana na mapatano yao, na kuungwa mkono na makundi mengineyo yenye silaha ya Kongo.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, Alan Doss, ameyahimiza makundi yote husika kuhakikisha raia huwa wanapatiwa hifadhi inayofaa, na kukumbusha juu ya majukumu yao chini ya sheria za kiutu za kimataifa kuhusu suala hilo. Alisema MONUC itaendelea kutekeleza madaraka iliodhaminiwa na Baraza la Usalama la kuyasaidia majeshi ya JKK kuwapatia hifadhi raia pamoja na ulinzi dhidi ya mashambulio. Kadhalika alisema MONUC itaendelea kuisaidia serikali kuunganisha wanamgambo wenye silaha na jeshi la taifa, na kuongeza bidii za kuwasilisha utaratibu wa kisiasa utakaotumiwa kurudisha hali ya utulivu nchini, na wakati huo huo kuwasaidia wahudumia misaada ya kiutu kuendeleza shughuli zao bila vizingiti.