Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, amekaribisha kidhati uamuzi wa serikali mpya ya Marekani, wa kufunga yale magereza yaliopo katika Ghuba ya Guantanamo, na vile vile kuunga mkono uamuzi wa kupiga marufuku taratibu zote zinazokiuka sheria ya kimataifa, zinazotumiwa na Marekani kusaili watu walio vizuizini. Vile vile Pillay alitoa mwito unaoitaka Marekani isitishe ile tabia ya kuteka nyara watu na kuwaweka vizuzini katika mataifa ya kigeni, kama vile Afghanistan na Iraq, na kupendekeza Marekani ikomeshe pia vitendo vya kutesa watuhumiwa kisiasa kwenye magereza ya nchi za nje.

Said Djinnit, mkuu waOfisi ya UM juu ya Afrika Magharibi Ijumatano aliwakilisha mbele ya Baraza la Usalama ripoti kuhusu hali kijumla na shughuli za taasisi yao kieneo. Alielezea athari za mgogoro wa chakula Afrika Magharibi, ikichanganyika na matatizo ya biashara haramu ya madawa ya kulevya pamoja na uhalifu wa mpangilio unaokiuka mipaka. Kadhalika, alihadharisha juu ya kupwelewa kwa utekelezaji wa mfumo wa kidemokrasia Afrika Magharibi baada ya kutukia mapinduzi katika Guinea na Mauritania.

Ijumatano Naibu KM wa UM Asha-Rose Migiro alihutubia kikao cha wajumbe wa Umoja wa Wabunge wa Mataifa Yanayozungumza Kifaransa, kilichofanyika kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York. NKM Migiro alipongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zinazotumia Kifaransa pamoja na UM, kwenye harakati za kuzuia, na kusuluhisha mizozo ya kimataifa, na vile vile katika kuendeleza mbele haki za kibinadamu na kuimarisha mifumo ya kidemokrasia, na pia katika kukuza maendeleo ya uchumi na jamii kimataifa. Alisema hivi sasa Taasisi ya Mfuko wa UM wa Kuimarisha Demokrasia inashirikiana na Umoja wa Wabunge wa Mataifa Yanayotumia Kifaransa kwenye utekelezaji wa ile miradi iliotayarishwa kuimarisha mifumo ya kidemokrasia katika Cambodia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Niger. NKM Migiro alisisitiza kazi za Umoja huo hufungamanisha vyema shughuli za serikali na raia na pia mahitaji ya kienyeji na yale ya kimataifa.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limetoa onyo lenye kuhadharisha kuzuka janga la viwavi vinayoangamiza mazao na mimea katika Liberia kaskazini, na inakhofiwa kama janga hili halijadhibitiwa haraka huenda likasambaa katika eneo zima la Afrika Magharibi, na kuzusha hali ya dharura mpya itakayosababisha upungufu wa chakula, mzoroto wa huduma za afya na uharibifu wa mazingira. Karibuni mtaalamu wa ilimu ya wadudu alitemebelea eneo husika la Liberia na aliripoti makumi milioni ya viwavi – vinavyotiliwa shaka vina asili ya mafunza wa KiAfrika – hula kilafi chochote wanachokikuta mbele yao. Katika baadhi ya sehemu za Liberia viwavi hivi viharibifu vilipamba majengo ya watu na kuwalazimisha wanakijiji, waliojaa khofu, kuyahama makazi na kukimbilia maeneo mengineyo kujisalimisha na wadudu hawo. Hivi sasa FAO imetayarisha timu maalumu itakayoshughulikia janga la viwavi haribifu katika Liberia na kuzingatia dawa zinazofaa kutumiwa kuwaangamiza wadudu.

Siku ya leo, tarehe 22 Januari 2009, inaadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa U Thant, KM wa tatu wa UM ambaye alitumikia tasisi ya kimataifa tangu 1961 mpaka 1971. Risala ya KM Ban, iliowakilishwa kwenye taadhima maalumu zilizofanywa mjini Yangon, Myanmar, taifa alipozaliwa U Thant, ilimsifu KM huyo kwa kuwa na mtazamo wa ushikamano wenye masilahi hakika ya jamii ya kimataifa. Alisisitiza katika kipindi chote cha maisha yake juu ya umuhimu wa kujifunza tamaduni anuwai zilizopo za kimataifa. Ilikuwa chini ya uongozi wa U Thant ndipo UM ulipoanzisha, kwa mara ya kwanza, ‘mwongo wa maendeleo’, na pia kubuni mashirika ya maendeleo ya UNDP, UNCTAD na UNIDO.