Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama lilikutana Ijumanne alasiri, kwenye kikao rasmi, kuzingatia hali katika Mashariki ya Kati na kusikiliza taarifa za Kamishna Mkuu wa Shirika la UNRWA, Karen AbuZayd, na John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu kuhusu tathmini yao kuhusu hali kwenye eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza kufuatia kusimamishwa mashambulizi na mapigano kieneo. Kadhalika, mapema leo hii Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Amani katika Mashariki ya Kati (UNSCO) iliripoti ya kuwa vivuko vyote baina ya Israel na Ghaza vinavyotumiwa na malori yanayoleta bidhaa na misaada ya kiutu, vilifungwa tena baada ya askari jeshi mmoja wa Israel kuuawa.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetoa Ripoti mpya ya Utendaji kuhusu Misaada ya Kiutu kwa 2009, ambayo iliangaza masaibu ya dharura za kiutu wanayokabiliwa nayo wanawake na watoto, matatizo ambayo yameonekana kusahauliwa kimataifa. Kadhalika UNICEF Imetoa ombi ya kutaka ifadhiliwe na wahisani wa kimataifa msaada wa dola bilioni moja ziada zinazohitajika kuhudumia masaibu ya dharura katika nchi 36, muongezeko ambao umejiri karibuni kwa sababu ya kuzidi kwa mahitaji ya kiutu katika kusini na mashariki katika Afrika. Kwa mujibu wa UNICEF zaidi ya nusu ya mchango huo ukipatikana utatumiwa kukidhi mahitaji ya umma wa mataifa ya JKK, Usomali, Sudan, Uganda na Zimbabwe.

Shirika la UM juu ya Utalii Duniani (WTO) limetangaza takwimu mpya leo zenye kueleza kwamba mnamo nusu ya pili ya 2008, shughuli za utalii ulimwenguni zilipwelewa, kwa sababu kadha wa kadha, ikijumlisha pia tatizo la kuzuka kwa mizozo ya fedha na kufumka kwa bei za nishati kwenye soko la kimataifa. Hali hii inaashiriwa itaselelea katika 2009 na kupita. Lakini licha ya mporomoko huo wa shughuli za utalii duniani, kuna maeneo machache ya ulimwengu yalioshuhudia matokeo ya kutia moyo, kuhusu jumla ya watu wanaotembelea sehemeu hizo katika 2008, ikijumlisha nchi kadha za Amerika ya Kati, na vile vile katika Jamhuri ya Korea (au Korea ya Kusini), pamoja na mataifa ya Bara Hindi, Morocco na Lebanon.