Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM atoa mwito wa kufadhiliwa dola milioni 613 kuhudumia Ghaza

KM atoa mwito wa kufadhiliwa dola milioni 613 kuhudumia Ghaza

Hii leo kutoka mji wa Davos, Uswiss – palipojumuika viongozi wa dunia kuzingatia masuala ya kufufua uchumi wa kimataifa – KM Ban Ki-moon alianzisha kampeni ya kuwaomba wahisani wa kimataifa kuchangisha, kidharura, dola milioni 613, zinazohitajika kuisaidia UM kuhudumia kihali na mali umma wa Tarafa ya Ghaza, ulioathirika na gharika na uharibifu wa wiki tatu wa eneo lao kutokana na mashambulio ya vikosi vya Israel.

“Bila shaka, kunahitajika misaada ya kihali haraka iwezekanavyo kwa umma wa Ghaza: kunahitajika chakula, maji safi na salama, makazi ya muda ya kujistiri, na vile vile kuna haja kubwa ya madawa na ufufuaji wa huduma za kimsingi.” KM alisema alipozuru Ghaza majuzi alishuhudia, binafsi, aina ya matatizo ya kihali yanayowakabili wakazi wa huko, ambao tangu hapo wameshateseka na vikwazo vilivyowekwa miezi kadha dhidi yao. Alisisitiza juu ya umuhimu wa kuanzisha, hivi sasa, kampeni ya kimataifa ya kuchangisha msaada wa dola milioni 613 kuhudumia maisha kwa wakazi wa Ghaza katika miezi sita ijayo. Alisema mchango huo utaiwezesha UM, ikichanganyika na mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu, kufanikiwa kuanzisha, haraka, miradi ya kuwanusuru kimaisha wakazi muhitaji milioni 1.4 wa katika Tarafa ya Ghaza.