Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumatatu, KM Ban Ki-moon ametangaza kumteua Michel Sidibé wa Mali, kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Jumuiya ya Kusimamia Miradi ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS). Sidibé anatazamiwa kuanza kazi tarehe 1 Januari 2009.

Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (DESA) imetangaza rasmi ripoti juu ya Matarajio na Hali ya Uchumi wa Dunia kwa 2009, kutokea mji wa Doha, Qatar. Ripoti iliwasilisha sura inayozingatia “Mwelekeo wa Uchumi Duniani”. Ilibashiria mporomoko kwenye uchumi wa kimataifa, utakaopambwa na maafa katika 2009, na kipindi baada ya mwaka huo. Ripoti ilisema ikiwa mbano wa shuruti za mikopo kwenye soko la kimataifa hautoregezwa mnamo miezi ijayo, nchi zenye maendeleo ya viwanda yatazama kwenye hali ya kudorora kwa uzito kabisa, kwa uchumi wao na, hatimayem, kuburura ukuaji wa maendeleo katika mataifa maskini, kwa kima ambacho kitahatarisha jitihadi za kupunguza umaskini na utulivu wa kisiasa kwenye maeneo yenye kushuhudia hali duni. Ripoti imependekeza kuchangishwa misaada maridhawa ya fedha itakayotumiwa kama vifurushi vya kufufua uchumi, na kurekibisha sheria kali za kudhibiti bora mifumo ya fedha na mageuzi mengine yanayotakikana kusawazisha huduma za uchumi wa kimataifa.

Shirika la UM Linalofarajia Huduma za Kiutu kwa Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) imeripoti kutofanikiwa kununua sarafu ya Israel ya shekel kuzipatia benki za eneo liliokaliwa kimabavu la WaFalastina katika Tarafa ya Ghaza. Matokeo yake ni kwamba UNRWA haitoweza kufadhilia misaada ya fedha kwa umma masikini sana 94,000 wanaotegemea huduma hizi kutoka UM. Kadhalika Shirika la UNRWA limesema linahitajia shekel 200,000 kuhudumia chakula watoto wa skuli 200,000. UNRWA hivi sasa inaendeleza shughuli za kuwapatia wanafunzi wa skuli misaada ya chakula, kwa mikopo, kutoka wachuuzi wa chakula, na imehhadharuisha kuwa italazimishwa kusitisha huduma hizo katika siku za karibuni, pindi UNRWA itashindwa kupatiwa fedha zinazohitajika kuendesha shughuli zake.

Croatia imekabidhiwa uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa mwezi Disemba. Balozi Neven Jurica ameanza mashauriano na wajumbe wa Baraza la Usalama kuandaa ajenda ya mwezi Disemba.