Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama kwenye kikao chake cha awali kwa mwezi huu, limepitisha ajenda ya kazi kwa Disemba. Baada ya hapo Baraza limepitisha azimio linaloruhusu, kwa muda wa miezi 12, Mataifa na mashirika ya kikanda kuingiza vyombo vyao katika maeneo ya mipaka ya bahari ya Usomali, kwa lengo la kukomesha vitendo vya uharamia na wizi wa kutumia silaha unaofanyika kwenye mwambao wa taifa hilo. ~~

Shirika la UM la Kusaidia Iraq la UNAMI, limewasilisha ripoti yake ya 13 juu ya haki za binadamu nchini, taarifa ambayo ilieleza kupatikana mafanikio makubwa, kwa ujumla, kuhusu udhibiti wa usalama katika nchi, licha ya kuwa mauaji ya raia walengwa yaliendelea katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya 2008, pamoja na kuendelea kwa vitendo vya kutorosha watu ambavyo majambazi baadaye hudai malipo kuwaachia mateka wao. Kadhalika ripoti ilisema jamii za wachache katika nchi zinaendelea kulengwa kutumiliwa mabavu dhidi yao, na kufanyiwa vitisho, mauaji pamoja na kuharibiwa mali zao na majengo ya kutunza utamaduni na mila zao.

Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani katika Mashariki ya Kati (UNSCO) imeripoti vile vivuko vinavyotumiwa kupelekea bidhaa katika Tarafa ya Ghaza vyote vinaendelea kuekewa vikwazo na vimefungwa sasa hivi, vikwazo ambavyo haviruhusu kupelekwa katika eneo liliozingiwa kimabavu na vikosi vya Israel mafuta ya petroli, vifaa vya kukidhia mahitaji ya kiutu na hata bidhaa za kibiashara.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti vitendo vya kutorosha watoto na kuwaingiza kimabavu kwenye majeshi ya mgambo bado vinafanyika na yale makundi yenye silaha katika Kivu Kaskazini. Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF karibuni watoto watano walilazimishwa kujiunga na makundi ya waasi katika mji wa Kitshanga. Kadhalika, iliripotiwea na UNICEF asilimia kubwa ya skuli kwenye eneo la Rutshuru zimefungwa, na kuwanyima haki ya kupata elimu ya msingi wanafunzi 150,000, ijapokuwa waasi wafuasi wa Jenerali Mtoro Laurent Nkunda waliahidi UM kuwa wataruhusu skuli hizo kufunguliwa. Makundi ya waasi yametakiwa yaandae mazingira ya utulivu, haraka, yatakayowaruhusu waoto kurejea skuli na kuendeleza masomo yao.

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 15, kwa aliyekuwa mwimbaji na mtunzi maarufu wa Burundi, Simon Bikindi, kwa kuchochea mauaji ya halaiki ya raia wenye jadi ya KiTutsi katika 1994. Waendesha mashitaka walithibitisha kwamba nyimbo na hotuba za uchokozi za Bikindi zilitumiwa wakati huo kuhamasisha kundi la waasi wa KiHutu wa Interehamwe, waliojumlisha pia wachezaji dansi za kuigiza hadithi wa kundi la wasanii aliomiliki Bikindi lilioitwa Irindiro, na waliendeleza mauaji ya halaiki kwa, kwanza, kujenga chuki dhidi ya raia wa KiTutsi katika wilaya ya Gisenyi.