Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa taarifa mpya kuhusu miripuko ya ugonjwa wa kipindupindu katika Zimbabwe, baada ya kufanyika mkutano maalumu, ulioitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Mtoto ya Zimbabwe, kikao ambacho kilihudhuriwa na maofisa wakazi wa WHO, Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) na mashirika mengine yaliopo nchini humo. Ripoti ya WHO

MONUC, shirika la UM juu ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), limearifu leo, Ijumatano, ya hali kuwa shwari sasa hivi katika eneo la mashariki. Wakati huo huo, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WHO) limeeleza kuongeza operesheni zake, za kupeleka misaada ya kiutu katika jimbo la Kivu Kaskazini na Jimbo la Orientale, ambapo raia hushambuliwa, mara kwa mara, na waasi wa Uganda wa LRA. Mnamo mwezi Novemba, WFP iliongeza misaada ya chakula kwa watu 564,000 katika eneo zina la mashariki, la JKK, na zaidi ya nusu ya idadi hii ilijumlisha wakazi wa Kivu Kaskazini, waliolazimika kuhama makwao kwa sababu ya mapigano. Lakini, watu 70,000 waliong’olewa makazi walishindwa kupelekewa misaada ya chakula,kwa sababu ya kuenea kwa hali ya wasiwasi na mtafaruku Kivu Kaskazini, na kutokana na barabara mbovu.

Shirika Linalosimamia Ulinzi Amani katika Liberia (UNMIL), kwenye ripoti yake kuhusu namna haki binadamu zinavyotekelezwa na kuhishimiwa nchini, ambayo hutolewa mara mbili kila mwaka, inasema maenedelo fulani yaliweza kushuhudiwa kwenye kadhia hiyo, ijapokuwa mfumo wa mahakama bado unahitajia kufanyiwa marekibisho, na unakabiliwa na vizingiti aina kwa aina kikazi, ikijumuisha lile tatizo la kutokuwepo watumishi wanaoaminika, kimsingi, kuhudumia sekta hiyo, pamoja na uhaba wa vifaa vya kuridhisha vinavyohitajia kusimamia, na kuendesha shughuli za taasisi za sheria. Ripoti ilisema vitendo vya utumiaji mabavu, vinavyohusishwa na udhalilishaji wa kijinsia, vimesalia katika jamii za Liberia; ikichanganyika na kuselelea kwa zile mila haribifu na hatari, ikijumlisha ada za kuua watu kutuliza mizimu na pepo, pamoja na tabia ya kutahiri watoto wa kike, mila ambazo huendelezwa kidhahiri bila kujali adhabu. UNMIL imependekeza misaada ya kiufundi ipelekewe Liberia na kutaka kuchukuliwe hatua ziada, zitakazosaidia kuimarisha zaidi mifumo ya mahakama nchini. Kadhalika, ndani ya ripoti, kulitolewa mwito wa kufanya kampeni, katika nchi nzima, kuwazindua raia na kuwahamasisha kukomesha ada haribifu na kufahamisha madhara yake kijamii na kimaadili. Halkadhalika, serikali ilitakiwa iruhusu Kamisheni Huru ya Taifa juu ya Haki za Binadaumu kuanza kufanya kazi zake bila ya kchelewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), Dktr Peter Piot ameripoti janga la UKIMWI bado halijamalizika, kamwe, katika bara la Afrika. Aliyasema hayo kabla ya kufunguliwa rasmi hii leo, mjini Dakar, Senegal kikao cha 15 cha Mkutano Mkuu wa Kimataifa juu ya UKIMWI na Maambukizo ya Magonjwa Yanayopatikana kwa Kujamiana. Kwa mujibu wa Jumuiya ya UNAIDS, eneo la Afrika kusini ya Sahara linaendelea kuwa ni sehemu ya kimataifa ilioathirika sana, na kudhurika zaidi na maambukizo ya virusi vya UKIMWI (VVU), ambapo inakadiriwa watu milioni 22 huishi, hivi sasa, na vijidudu hatari hivyo. Katika 2007, eneo la Afrika kusini ya Sahara lilijumlisha thuluthi mbili ya watu wote wenye kuishi na VVU, na ndipo palipotukia robo tatu ya jumla ya vifo vyote vya UKIMWI duniani. Ugonjwa wa UKIMWI, ilisisitiza taarifa ya UNAIDS, ndio wenye kuongoza katika kusababisha vifo katika Afrika.