Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

~ Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah ameripoti kutafanyika Mkutano wa Kimataifa juu ya Uharamia katika Usomali kwenye mji waNairobi, kuanzia Ijumatano mpaka Alkhamisi wiki hii. Maofisa 140 kutoka nchi 40, pamoja na wale wanaowakilisha mashirika ya kikanda na ya kimataifa, wanatazamiwa kuwa miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano. ~

Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani Mashariki ya Kati imetangaza kwamba baadhi ya bidhaa, ziliruhusiwa Ijumanne kuingia Tarafa ya Ghaza kutokea Israel, zikijumlisha shehena ya misaada ya unga, iliobebwa kwenye malori kumi, itakayotumiwa na Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kugawa chakula kwa umma muhitaji. Shirika la UM Kufarajia Mahitaji ya Kihali kwa Umma wa Falastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) nalo pia lilifanikiwa kupokea malori matatu yaliobebeshwa nyama za kibati, na malori matatu mengine yaliokuwa yamechukua nyama za vibati kwa umma wa Ghaza. Wakati huo huo, mkutano wa kila mwaka, kuchangisha misaada ya kihali kwa wahamiaji wa KiFalastina kwa 2009, utafanyika Ijumatano ya tarehe 10 Disemba (2008), kwenye Makao Makuu mjini New York. Kwa mujibu wa taarifa ya UNRWA kunahitajika msaada wa dola milioni 550 kwa 2009 kutoka wahisani wa kimataifa, msaada ambao utatumiwa kuendeleza shughuli za UNRWA za kukidhia mahitaji ya ilimu, afya, misaada ya kijamii na mikopo ya ushuru mdogo kwa Wafalastina muhitaji milioni 4.6 waliosajiliwa na UNRWA.

Ripoti iliotolewa bia Ijumatatu na Shirika la Miradi ya Chakula na Kilimo (FAO), pamoja na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), imebainisha asilimia 40 ya idadi ya watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK), yaani Korea ya Kaskazini – wanaokadiriwa milioni 4.7 – wingi wao wakiwa watoto wadogo, mama waja wazito na wale wanaonyonyesha, pamoja na watu wa umri mkubwa, watahitajia kufadhiliwa misaada ya dharura ya chakula mnamo miezi ijayo kwa sababu ya sekta ya kilimo haitomudu kuzalisha mavuno ya sayari nchini yanayohitajika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya chakula kwa raia.