Skip to main content

Wenye njaa ulimwenguni wamekithiri katika 2008, inasema ripoti ya FAO

Wenye njaa ulimwenguni wamekithiri katika 2008, inasema ripoti ya FAO

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limeeleza, kwenye ripoti rasmi iliotolewa Ijumanne, kuhusu hali ya chakula kimataifa kwa 2008, kwamba idadi ya watu wenye njaa sugu ulimwenguni imekithiri pakubwa,kwa sababu ya mifumko ya bei za chakula duniani.

Takwimu za ripoti mpya ya FAO kuhusu tatizo la njaa ulimwenguni, iliochapishwa Roma, Utaliana hii leo, imethibitisha kwamba watu milioni 40 wamezamishwa kwenye janga la njaa mwaka huu, kwa sababu ya kupanda, kwa kasi, kwa bei za chakula. Jumla ya watu wanaokosa chakula cha kutosha kuishi ulimwenguni imekadiriwa kufika watu bilioni 1 kwa mwaka huu, sawa na watu milioni 963. Mwaka jana, katika kipindi kama hiki cha sasa, jumla ya watu waliosibiwa na njaa ilisajiliwa kuwa milioni 923. Hafez Ghanem, Mkurugenzi-Mkuu Msaidizi wa FAO alinakiliwa akisema “ni ndoto ya mbali sana, kwa mamilioni ya watu wa nchi nchi zinazoendelea, kufikiria watapatiwa uwezo wa chakula cha wastani, kila siku, kitakachowawezesha kumudu shughuli za maisha na kutunza afya bora.” Matatizo ya kimfumo yanayochochea njaa, mathalan, ukosefu wa rasilmali ya ardhi ya kilimo, ukosefu wa ajira na mikopo, ikichanganyika na bei ghali ya chakula,” ni mambo ambayo FAO inasema hayawezi kukanushika, na yanadhihirisha hali hakika ilivyo kimataifa. Ripoti ya FAO ilipewa mada isemayo “Hali ya Wasiwasi wa Chakula Duniani kwas 2008.”