Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Mdogo Msaidizi juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM, Edmond Mulet anazuru Cote d’Ivoire wiki hii, ambapo alikutana na Raisi Laurent Gbagbo kwenye mji wa Yamoussoukro na walijadilia huduma za katika nchi za Shirika la Ulinzi Amani la UM la UNOCI. Idhini ya kuendeleza operesheni za amani za UNOCI, iliotolewa na Baraza la Usalama, itamaliza muda wake mnamo mwisho wa Januari 2009, na Mulet anafanya tathmini ya kiufundi kuhusu shughuli za UNOCI. Vile vile Mulet anatarajiwa kukutana na viongozi wa kisiasa wanaowakilisha vikundi mbalimbali nchini, miongoni mwao wakijumuisha Alassane Ouattara na Henri Konan Bédié.

Ofisi ya Mratibu Maalumu juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati (UNSCO) imeripoti malori 93 yaliruhusiwa Alkhamisi kuingia Tarafa ya Ghaza na Israel, na malori 21 kati ya jumla hiyo yalikuwa ya mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu kwa WaFalastina. UNSCO imekumbusha ya kuwa idadi wastani ya malori yenye kubeba bidhaa, yaliokuwa yakiruhusiwa kuingia Ghaza katika mwezi Oktoba, ilikuwa malori 123 kwa siku. Mwezi Mei malori 475, yenye kubeba bidhaa za kukidhi mahitaji ya umma wa Ghaza, yaliruhusiwa kuingia kwenye eneo hilo kila siku. Takwimu hizo zinabainisha jumla ndogo ya malori yalioruhusiwa kuingia Ghaza katika tarehe ya leo, yaani 11 Disemba 2008, tukilinganisha na miezi iliopita. Shirika la UM Linalofarajia Misaada ya Kihali kwa Wahamiaji wa Dharura wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), kwa upande wake limearifu kupokea malori saba hii leo yalioruhusiwa kuingia Ghaza na shehna ya sukari, nyama ya vibati na unga wa maziwa, vitu ambavyo vitagaiwa umma muhitaji wa KiFalastina.

Staffan de Mistura, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Iraq ameripoti wasiwasi juu ya hali na usalama wa wafanyakazi wa kigeni 1,000, walioajiriwa na kuingizwa nchini na makandarasi wa kimataifa. Wafanyakazi hawa imeripotiwa wameachwa sasa hivi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. De Mistura alisema madai ya kuwa wafanyakazi hawa wametoroshwa, na hawakujua walipokwenda, wakitumai kuajiriwa kazi, ni tuhumu zenye kuashiria dosari mbaya kabisa juu ya vitendo vya makandarasi. Alidhihirisha kwamba UM umeshakamilisha uchunguzi na tathmini huru kuhusu hali ya wafanyakazi walionaswa kwenye Kiwanja cha Ndege cha Baghdad, na maofisa wa UM wameshauriana na wenye madaraka husika pamoja makandarasi waliopo Iraq, kwa madhumuni ya kuhakikisha kanuni za haki za wafanyakazi za kimataifa zinatekelezwa na kuhishimiwa kuhusu wafanyakazi husika.