Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa kimataifa wakusanyika Poland kuzingatia udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa

Wajumbe wa kimataifa wakusanyika Poland kuzingatia udhibiti wa mabadiliko ya hali ya hewa

Mawaziri wa mazingira na wawakilishi wa ngazi za juu wa kiserikali, kutoka karibu nchi 200, wamekusanyika Alkhamisi ya leo kwenye mji wa Poznan, Poland kuhudhuria kikao cha kuzingatia hatua za kimataifa, za kuharakisha maafikiano ya pamoja, yatakayotumiwa kudhibiti bora matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Mkutano wa Poznan umejumuisha wajumbe wa kimataifa 11,600 na umeshafikia kile kipindi cha nusu ya majadiliano ya kuandaa ratiba ya kuridhisha, kuhusu hatua za kuchukuliwa kimataifa dhidi ya uharibifu unaoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, maafikiano yanayotazamiwa kukamilishwa mwisho wa 2009 kwenye mkutano utakaofanyika Copenhagen, Denmark ambapo mataifa yataridhia chombo mbadala cha kisheria kitakachotumiwa rasmi kuanzia 2013 kudhibiti mabadiliko ya hali yahewa, mwaka mmoja baada ya Mkataba wa Kyoto kumaliza muda wake.