Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ofisi ya UM ya Mratibu Maalumu juu ya Mpango wa Amani Mashariki ya Kati (UNSCO) imeripoti kinu cha taa/umeme cha Tarafa ya Ghaza, ambacho hukidhi baadhi ya mahitaji ya eneo, kimefungwa kukhofia kisije kikaharabika zaidi kutokana na kuwashwa na kuzimwa mara kwa mara, kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kuendeshea mtambo wa umeme. Baadhi ya sehemu za Ghaza hukoseshwa umeme kila siku kwa saa 12, na maeneo mengine hukosa umee kwa saa 4 kila siku. UNSCO imeripoti pia malori 81 yaliruhusiwa Ijumatatu kuingia eneo la Tarafa ya Ghaza, kutokea Israel, yakijumlisha pia malori 20 ya mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu. Malori ya mashirika ya UM yalibeba shehena ya unga, maziwa, madawa na vitu vyengine kukidhia mahitaji ya watumishi wao.

Mnamo asubuhi ya tarehe 15 Disemba 2008, KM wa UM, aliongoza kikao cha sita cha Tume Maalumu ya Hadhi ya Juu Kuzingatia Mzozo wa Chakula Duniani. Wajumbe wa Tume walikubaliana ajenda kwa 2009, ambayo inalenga zaidi juhudi za kimataifa kwenye taratibu za kupunguza njaa, kuimarisha akiba maridhawa ya chakula na kupanua kilimo cha wakulima wadogo wadogo katika zile nchi zinazohitajia msaada huo. KM alitangaza kwamba ameafikiana na Waziri Mkuu wa Uspeni, Jose Luis Rodriguez Zapatero, kusimamia bia mkutano wa cheo cha juu, utakaofanyika Madrid, Uspeni kuanzia tarehe 26-27 Januari 2009 kuzingatia “Chakula kwa Wote”. Wajumbe wa serikali, taasisi za binafsi na makundi ya jumuiya za kiraia wanatarajiwa kutatathminia maendeleo katika kudhamini bora chakula, kuchanganua ramani ya siku za usoni kukuza chakula na kukabiliana na tatizo la njaa kwa mwelekeo unaofaa na wenye natija.

Alasiri KM aliwakilisha taarifa maalumu kwenye kikao cha faragha katika Baraza la Usalama, kuhusu hali Zimbabwe. Kadhalika, Baraza la Usalama lilipokea ripoti maalumu kutoka tume za usaidizi na kufanya mashauriano kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Ijumamosi, Baraza lilikutana kushauriana mswada wa azimio linalozingatia hali ya amani Mashariki ya Kati, azimio ambalo litajadiliwa kwenye mkutano rasmi utakaofanyika Makao Makuu Ijumanne.

UM imeripoti idadi ya wagonjwa wa kipindupindu Zimbabwe sasa imekiuka 18,000 (18,413) na kati ya hawo 978 walishafariki. Mripuko wa maradhi sasa umeathiri majimbo tisa kati ya kumi katika Zimbabwe, na yamefurikia Afrika Kusini, Msumbiji na Botswana.

Francis Deng, Mshauri Maalumu wa KM kuzuia mauaji ha halaiki amerejea Makao Makuu baada ya ziara ya siku 12 katika mataifa ya Maziwa Makuu. Allipokuwepo JKK, Rwanda na Uganda Deng alikutana na maofisa wa serikali na wale wa UM, pamoja na wawakilishi wa jumuiya za kiraia, watumishi wa makanisa na waathirika wa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu. Wajumbe wengine wa tume ya Deng walizuru Burundi vile vile kuendeleza shughuli hizo hizo, wakati Deng alipokutana na viongozi wa baadhi ya makundi makuu ya wanajeshi wa mgambo katika mashariki ya JKK.

Shirika la Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limearifu asilimia 90 ziada ya wanajeshi wa UM sasa hivi wameenezwa kwenye majimbo ya kaskazini-mashariki ya nchi. Hali ya usalama katika maeneo haya inasemekana kuwa ni ya shwari, na askari jeshi 6,200 wa UM wanafanya doria ya nguvu Kivu Kaskazini, wakati askari 1,000 wamesambazwa eneo la Goma pekee. Wanajeshi wengine 3,500 wametawanywa Kivu Kaskazini na 3,800 wanafanya doria zao katika mji wa Ituri. Wanajeshi waliosalia wa UM wanaendeleza shughuli zao za kulinda amani kwenye sehemu nyengine za nchi, ikijumlisha mji wa Kinshasa.

Kwenye hotuba aliowasilisha mbele ya Baraza Kuu la UM asubuhi ya leo, Naibu KM Asha-Rose Migiro alieleza kuingiwa moyo juu ya uhamasishaji wa kimataifa kuhudumia Miradi ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Hata hivyo, aliyasihi Mataifa Wanachama kutopwelewa katika kuzitekeleza zile ahadi walizotoa kuyakamilisha Malengo ya MDGs kama inavyopaswa. Alisema huu ndio wakati wa “kuwa wamoja” na kutumia kila fursa, katika mwaka ujao wa 2009, kuhakikisha usumbufu uliopo hautotuvuta mbali na majukumu ya pamoja , hususan katika kukamilisha yale malengo yanayohusu “juhudi za kuimarisha amani na ustawi wa maendeleo kwa wote.”