Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumanne alasiri Baraza la Usalama limepitisha azimio, liliothibitisha wazi kuunga mkono majadiliano yalioanzishwa mwaka jana kwenye mji wa Annapolis, Maryland, Marekani kuhusu suala la amani baina ya Waisraili na WaFalastina. Vile vile azimio limeahidi kuhakikisha mazungumzo ya pande mbili, baina ya Waisraili na WaFalastina, hayatotenguliwa wala kubadilishwa. Azimio liliodhaminiwa bia na Marekani na Urusi lilipitishwa na mataifa 14 kati ya wajumbe 15 wa Baraza. Libya iliamua kutopiga kura.

Ijumanne alasiri, kwenye kikao rasmi cha hadhara, Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio kuhusu ushirikiano wa kimataifa kwenye juhudi za kukabiliana na uharamia na wizi unaotumia silaha kwenye maeneo ya bahari nje ya mwambao wa Usomali. Wakati huo huo, Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu imependekeza hatua kadha kuchukuliwa kukabilaina na uharamia kwenye eneo la Pembe ya Afruika.

Vikosi Mseto vya Kulinda Amani Darfur vya UM-UA (UNAMID) vimeripoti kupelekwa timu maalumu ya uchunguzi Darfur Kusini baada ya taarifa za kuzuka mapigano ya kikabila kieneo.

Kadhalika, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kundi la raia 97 wa Sudan, wingi wao kutokea Darfur, walionaswa tangu 2005 kwenye kambi za muda katika jangwa la Iraq, wamepelekwa Amman, Jordan leo asubuhi, ambapo wanatarajiwa kuchyukua ndege zitakazowapeleka uhamishoni Romania. Watakapofika Romani wanatarajiwa kuwekwa kwenye Kituo cha Mpito cha Dharura wakati wakisubiri jawabu ya maombi yao ya hifadhi ya kisiasa. Wahamiaji hawa wa Sudan walipokuwa Iraq waliteswa na majeshi ya mgambo, ambayo pia yaliowanyanyasa, yaliwasaliti, na kuwafukuza mastakimu na vile vile kuwashambulia kwa vitisho na mapigo. UNHCR ilithibitiha baina ya Disemba 2004 mpaka Februari 2005 jumla ya WaSudani 17 waliuawa Iraq.

Maduka maarufu ya IKEA yametangaza kwamba – kuanzia sasa hadi tarehe 24 Disemba – itafadhilia Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) uro moja kwa kila vitu vya kuchezea. Mchango huo utatumiwa kuhudumia miradi ya ilimu inayoendeshwa na UNICEF pamoja na lile shirika lisio la serikali la Save the Children.

Raisi Migeule D’Escoto ameliambia Baraza Kuu la UM leo hii kwamba mizozo ya kimataifa iliojiri ulimwennguni kwa sasa, kuanzia migogoro ya chakula, matatizo ya fedha kwenye soko la kimataifa na ughali wa nishati, ni matukio yanayowakilisha fursa ya kukuza ushikamano na umoja wenye natija miongoni mwa mataifa yanayoendelea. Alisisitiza natija ziliopo zitasaidia kuimarisha ushirikiano bora wa kiuchumi kati ya mataifa yanayoendelea, yaliopo Kusini ya Ikweta. Risala hii ya D’Escoto iliwasilishwa kwenye kikao maalumu cha Siku ya UM juu ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kusini, siku ambayo huadhimishwa rasmi kimataifa katika tarehe 19 Disemba.