Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yalaani mauaji ya mtumishi wa AVSI katika JKK, na kuchukizwa na mizungu ya wafuasi wa Nkunda

UNHCR yalaani mauaji ya mtumishi wa AVSI katika JKK, na kuchukizwa na mizungu ya wafuasi wa Nkunda

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetangaza kuchukizwa na mauaji ya kikatili, yaliotukia jana Ijumatatu katika jimbo la Kivu Kaskazini, katika JKK, dhidi ya mfanyakazi wa shirika lisio la serikali la Kitaliana, linaloitwa Jumuiya ya Hiari kwa Huduma za Kimataifa (AVSI).

UNHCR inasikitika na mauaji ya kikatili ya mtumishi wa Jumuiya [ya Kitaliana] ya Hiari kwa Huduma za Kiutu Kimataifa (AVSI), yaliotukia Kivu Kaskazini karibu na mji wa Rutshuru Ijumatatu alasiri … ambapo mtu mwenye silaha, alishambulia kwa kuvizia, gari iliokuwa imechukuwa watumishi wa AVSI, na kumwua mmoja wa wafanyakazi wa AVSI, na kumjeruhi mwenziwao mmoja mwengine.” Kwa mujibu wa Redmond, shambulio lilitukia nje ya Rutshuru, kilomita 80 kaskazini ya mji wa Goma. Vile vile alisema UNHCR ina wasiwasi na ripoti ilizopokea juu ya vitisho na unyanyasaji unaoendelezwa na wafuasi wa kundi la waasi la Jenerali Mtoro Laurent Nkunda, dhidi ya wahamiaji 10,000 wa ndani waliokuwa wakitafuta hifadhi ya maisha, karibu na kambi ya Rutshuru ya Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC). Wafuasi wa Nkunda inaelekea wanawalazimisha, kwa vitisho na silaha, wahamiaji hawa kurejea vijijini kwao bila hiari, na hata huwazuia, kwa nguvu, kwenda kwenye vituo vya MONUC kuomba hifadhi. Kadhalika, imeripotiwa wafuasi wa Nkunda wanaajiri vijana wadogo kuendeleza doria za usiku na kutumia mabavu dhidi ya wanavijiji ili wasiende kuomba ulinzi kwenye kambi za UM za MONUC.