Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM Kulinda Amani katika JKK (MONUC) limearifu Ofisi juu ya Ukaguzi wa Makosa ya Kikazi (OIOS) inaendeleza uchunguzi kuhusu tuhuma za kuwa baadhi ya wahudumia amani katika eneo la Kivu Kaskazini walishiriki kwenye vitendo vibaya dhidi ya raia. MONUC insasema baadhi ya vitendo hivyo hujumuisha ukandamizaji na udhalilishaji wa kijinsiya. MONUC iliongeza kusema kwa kuhadharisha ya kwamba hadi sasa hivi tuhumu hizo ni madai ambayo bado hayajathibitishwa kisheria. Watumishi wote wa MONUC wamenasihiwa kushirikiana kikamilifu na wachunguzi wa Ofisi ya OIOS.

Baraza Kuu la UM limemaliza mijadala ya kikao cha 63, kwa mwaka huu, katika saa kumi za alfajiri ya Ijumatano, ambapo wajumbe wa kimataifa walipitisha azimio la kuongeza, kwa asilimia 17, fedha ziada kwenye bajeti la 2008-2009, jumla ambayo ni sawa dola bilioni 4.87 badala ya dola bilioni 4.17 zilizopitishwa hapo kabla. Bajeti jipya linajumuisha mchango wa dola karibu milioni 500 ziada, fedha ambazo zinahitajika kuhudumia operesheni za ulinzi amani kwenye lile jimbo la vurugu la Sudan magharibi la Darfur, katika miezi sita ijayo. Azimio hili lilikuwa miongoni mwa maazimio kadha mengineyo yaliopitishwa, kwa kufuatana na mapendekezo ya Kamati ya Tano ya Baraza Kuu, yaani ile Kamati Inayohusika na Usimamiaji wa Utawala na Bajeti la kuendesha shughuli za UM. Raisi wa Baraza Kuu Miguel D’Escoto alipofunga mkutano aliyahimiza Mataifa Wanachama kuutumia wakati ujao wa mapumziko kabla ya mwaka mpya “kuchaji tena betri”, na kuhakikisha watakaporejea kwenye kazi katika 2009 watarudi na “bidii itakayokuwa na nguvu mpya” ya kukabiliana vilivyo na masuala muhimu juu ya ustawi wa kimataifa. KM Ban Ki-moon, kwenye risala alioitoa, kwa kupitia msemaji wake aliwashuruku, binafsi, wajumbe wa Mataifa Wanachama kwa kupitisha bajeti ambalo anaamini litatusaidia kuwa na uwezo wa kudhibiti vyema mahitaji ya UM” katika kipindi kijacho.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNCEF) limetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za pamoja, za kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na mauaji ya karibuni ya watu mazeruzeru katika Tanzania. Ripoti zilizopokelewa kutoka Jumuiya Mazeruzeru Tanzania inasema mazeruzerui 35 ziada waliuawa Tanazania mwaka huu, na inakhofiwa kulikuwepo mauaji mengine zaidi ya mazeruzeru ambayo hajaripotiwa na wenyeji, hususan wale wanaoamaini damu na viungo vya mazeruzeru vina miujiza ya kuwatajirisha. Vitendo hivi katili sasa vimenea pia katika taifa jirani la Burundi. Kwa mujibu wa taarifa za UNICEF wenye madaraka Tanzania wamefanikiwa kuwashika watu 173, wakijumlisha askari polisi watano, waliotuhumiwa kuhusuiana na mauaji ya mazeruzeru. Kadhalika, Serikali ya Tanzania inaripotiwa kutoa hifadhi, hivi sasa, kwa raia mazeruzeru, katika sehemeu zote za nchi. Raisi wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameripotiwa kulaani mashambulio dhidi ya mazeruzeru na amependekza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wauaji. UNICEF imezipongeza hatua hizo za Tanzania na kuhimiza pia mahakama, vyombo vya habari, viongozi wa kidini, wanasiasa na vile vile jamii kuilimisha umma, kwa ujumla, dhidi ya uovu wa itikadiza kikale zinazochochea mauaji ya mazeruzeru.

Wiki hii Ujerumani imeshitaki kwenye Mahakama ya Kimataifa (ICJ) iliopo Uholanzi, dhidi ya Utaliana, taifa ambalo, ilisema mahakama zake bado zinaruhusu kutoa maamuzi ya kullipwa fidia waathirika wa makosa ya jinai ya vita, yalioendelezwa na utawala wa Kinazi wa miaka mingi iliopita. Ujerumani ilisisitiza kwenye ombi la mashitaka ya kuwa maamuzi ya Utaliana, yanakwenda kinyume na mikataba ya kimataifa, kwa sababu Ujerumani imeshalipa fidia halisi kwa wale walioathirika na utawala wa Kinazi. Kadhalika, Ujerumani ilisisitiza kwamba ilivyokuwa ni Taifa huru, haliwajibiki tena, kisheria, kutekeleza hukumu dhidi yake, hisisan zile zinazotolewa na mahakama za Kitaliana, na kukumbusha ya kuwa uamuzi wowote wa mahakama za Kitaliana dhidi ya Ujerumani hauna nguvu na hautekelezeki. Licha ya hoja zote hizi, Ujerumani ililalama, mfumo wa sheria katika Utaliana si sawa maana bado unaendelea “kuvunja na kukiuka” haki halali za Ujerumani, na kuharamisha uhuru wake, kwa kukubali kupokea kesi mpya za wale wenye kudai fidia dhidi ya Taifa la Ujerumani kwa sababu ya jinai iliofanywa wakati wa utawala wa Kinazi zaidi ya miaka sitini iliopita.