Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lahimiza uhasama na vurugu usitishwe Ghaza

Baraza la Usalama lahimiza uhasama na vurugu usitishwe Ghaza

Baada ya majadiliano ya karibu saa tano, kwenye kikao cha dharura, wajumbe wa Baraza la Usalama waliokutana Ijumapili, alfajiri, waliafikiana kutoa taarifa maalumu kwa waandishi habari kuhusu hali ya vurugu lilioripuka Ijumamosi katika Tarafa ya Ghaza, eneo la Wafalastina liliokaliwa kimabavu .

Karen AbuZayd, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) kwenye taarifa aliotoa tarehe 27 Disemba 2008 alieleza “mshtuko” aliopata kuhusu “uharibifu mkubwa uliogharikisha eneo la Tarafa ya Ghaza” na alisema ana "huzuni kuu kuhusu upotezaji maisha uliotokea kwa wanadamu wanaoishi huko.” Aliinasihi Serikali ya Israel kusitisha “mashambulizi yote ya mabomu Ghaza” na kuikumbusha jukumu iliodhaminiwa kisheria la kuhakikisha raia, wasioshiriki kwenye mapigano, huwa wanapatiwa hifadhi na ulinzi, kwa kulingana na mikataba ambayo, alisistiza, Israel imeshaiwekea sahihi na kuiridhia. Abu Zayd alisema pindi mikataba hii ya kimataifa ya kulinda raia haitohishimiwa na yale mataifa yalioiridhia, itamaanisha sheria hizi za kimataifa huwa hazina thamani na hazifai kitu!