Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon ametangaza kumteua tena Liuteni-Jenerali Babacar Gaye wa Senegal kuwa Kamanda Mkuu wa Dharura wa Vikosi vya MONUC kwa miezi sita ijayo. Lengo la uteuzi huo wa Jenerali Gaye ni kukabiliana vyema na matatizo yaliozuka Kivu Kaskazini katika JKK. Jenerali Gaye alikuwa Kamanda Mkuu wa MONUC kuanzia March 2005 hadi Oktoba 2008.

Kwa wakati huo huo, Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti “makundi yenye silaha” yamegunduliwa yakizurura kwenye kambi mbili za UM zilizokuwa zikitumiwa kuwahifadhi wahamiaji wa ndani (IDPs) nchini. Kambi hizi zipo kilomita 10 kaskazini ya Goma. OCHA imeripoti wahamiaji waliokuwa na khofu walitelekezwa kutoka kambi hizo. Kadhalika, UM umeripoti uchunguzi wa kambi za Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) ziliopo mji wa Rutshuru ziliionekana tupu, na wingi wa makazi yalichomwa moto, na haijulikani ni mahali gani wakazi wake walipoelekea.