Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kuzuka tena, kwa vipindi, mapigano, katika eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), baina ya jeshi la mgambo la kikabila, linaloitwa PARECO, na waasi wafuasi wa Jenerali Mtoro, Laurent Nkunda. Vurugu hili limekomea kwenye kijiji cha Kiwanja, kilomita mbili nje ya eneo la Rutshuru ambalo sasa hivi limekaliwa na waasi. Vile vile MONUC imeeleza wanajeshi wa UM waliopo kwenye kambi jirani, wamejikuta wamenaswa katikati ya mazingira ya mapigano. Licha ya hayo, mpaka sasa hakujaripotiwa mtu kujeruhiwa, isipokuwa kuna wasiwasi kila mapigano yakiselelea huenda yakasababisha uharibifu mkubwa wa kambi hizo. Wahudumia misaada ya kiutu pamoja na wale wanaotathminia mahitaji ya umma wamelazimika kusitisha huduma zao hizo, mpaka mapigano yatakapositishwa kikamilifu. ~

Makubaliano ya kusitisha mapigano miongoni mwa makundi yanayohasimiana Goma yanaoenekana yanaendelea kuhishimiwa. Kombania mbili za majeshi ya ulinzi amani ya UM zimewasili Goma Ijumanne, na vikosi vya polisi vinatazamiwa kutawasili huko Ijumatano. Hivi sasa katika jimbo la Kivu Kaskazini wameenezwa wanajeshi 5,000 wa UM, na askari 1,700 kati ya hawo wapo Goma pekee.

Wakati huo huo, Alain Le Roy, mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM (DPKO), pamoja na Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Alan Doss, walienedelea na ziara yao leo Ijumanne katika Kivu Kaskazini. Walizuru kambi za watu waliong’olewa makazi na vile vile vituo vya wanajeshi wa UM, kabla ya kuwatembelea watumishi wanaohudumia misadaa ya kiutu waliopo kwenye eneo hilo. Kadhalika walikutana na Waziri Mkuu na wawakilishi wa kimataifa waliopo huko wakijihusisha na zile juhudi za pamoja za kuleta amani ya eneo – wakijumlisha wajumbe wa kutoka Umoja wa Ulaya na pia Marekani.

Vikosi vya Mchanganyiko vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa Darfur (UNAMID) viliripoti vilifanikiwa kupeleka vifaa, zana na magari yanayohitajika kutumiwa kudhibiti bora amani katika Darfur. Huu ni msafara wa tisa wa vifaa hivyo vilivyosafirishwa kilomita 900 kutokea kituo cha El Obeid hadi Darfur. Msafara ulijumlisha magari 39, yakiwemo malori saba yaliobeba vifaa vya wanajeshi na malori matatu yaliokuwa yamechukua misaada ya kiutu. Msafara ulipitia kwenye ardhi zilizo mbaya mno, ambazo huwa hazipitiki kabisa wakati wa majira ya mvua. UNAMID ilisema msafara kama huo huwapatia fursa polisi wa UM kuwasiliana na wenyeji kwenye vijiji kadha wa kadha, na vile vile kujenga mafahamiano bora na polisi wa kizalendo.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetoa taarifa yenye kulaani vikali kitendo cha kupigwa mawe mpaka kufa kwa binti wa miaka 13 wa Kisomali, anayeitwa Aisha Duhulow, ambaye alituhumiwa zinaa. Tukio hili lilijiri wiki iliopita baada ya mahakama ya KiIslamu kutoa hukumu hiyo katika mji wa Kismayo. Kwa mujibu wa UNICEF ripoti ilizopokea zinadai binti huyo alisumbuliwa, kutishwa na baadaye kunajisiwa kimabavu na wanaume watatu watu wazima. Walimshika binti baina ya Kisamyo na Mogadishu, wakati alipokuwa akielekea kuzuru jamaa zake. UNICEF ilikumbusha tena kwamba watoto wa kike na wanawake katika Usomali wanakabiliwa na hali ya hatari kimaisha, wakati wote, hali ambayo huwakuta wanadhalilishwa na kutumiliwa mabavu dhidi yao kwa sababu ya ubaguzi wa kijinsia. Maafa haya mara nyingi hupaliliwa zaidi na migogoro sugu ilioselelea nchini pamoja na msiba wa kung’olewa makwao waathiriwa hawo.