Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

FAO na UM leo inaomboleza, kwa huzuni kuu, kifo cha ghafla Ijumapili (09/11/2008) cha mwanaharakati wa haki za binadamu na mwimbaji maarufu wa Afrika Kusini, Miriam Makeba. Tangu 1999 Makeba alikuwa Balozi Mfadhili wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) kwenye kampeni ya kukomesha tatizo la njaa, na alishiriki katika tafrija mbalimbali zilizoandaliwa na UM. Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jacques Diouf alisema kwenye taarifa rasmi kufuatia tangazo la kifo kwamba marehemu Makeba alikuwa mtetezi, aliojitoea kwa dhati, kupigania ukomeshaji wa njaa kimataifa. Mwezi Machi alizuru miradi ya dharura ya FAO Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambayo iliandaliwa kuwasaidia waathiriwa wa vurugu pamoja, na kuwasaidia wanaume na wanawake walioambukizwa na virusi vya UKIMWI kuwapatia chakula aila zao kwa kuwaajiri kwenye sekta ya kilimo.~

Vikosi vya Mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID), vilivyowakilisha wanajeshi wa Nigeria, vilishambuliwa kwa kuvizia, Ijumapili alasiri, na kundi la watu wasiotambulikana waliokuwa wamechukua makombora ya roketi pamoja na bunduki za aina ya AK-47, wakati walipokuwa wakifanya doria katika eneo la Darfur Magharibi. Askari mmoja aliyejeruhiwa anatibiwa sasa hivi kwenye hospitali ya UNAMID, iliopo El Fasher, Darfur Kaskazini. UNAMID imeshtumu vikali shambulio iliosema ni la kiwoga na uchokozi. Wakati UNAMID inaendeleza uchunguzi juu ya tukio hilo imeyakumbusha makundi yote husika kwenye eneo la operesheni zao za kijeshi ya kwamba, kwa kulingana na sheria ya kimataifa mashambulio ya aina yeyote dhidi ya walinzi amani hutambuliwa kama ni makosa ya jinai ya vita.