Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) linajitayarisha sasa hivi kuongeza mara mbili zaidi idadi ya watu watakaohudumiwa chakula mwezi Novemba nchini Zimbabwe; na kwa wakati huo huo WFP imetahadharisha italazimika kupunguza posho ya chakula inayogawa kwa umma Zimbabwe kwa sababu ya upungufu wa fedha za kukidhia mahitaji yao. Hivi sasa WFP imeomba ifadhiliwe na wahisani wa kimataifa msaada wa dola milioni 140, fedha zinazohitajika kuendesha operesheni zake kuanzia kipindi cha sasa hadi mwisho wa Machi 2009. Mnamo mwezi Oktoba, kipindi ambacho WFP ilipoanzisha operesheni zake kubwa za kugawa chakula Zimbabwe, ilifanikiwa kugawa tani 29,000 za posho za chakula kwa umma unaokadiriwa milioni mbili.~

Ijumatatu maofisa wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) walizuru tena zile aila za Wakristo wa Iraq katika Mosul, raia ambao mwezi Oktoba walilazimika kuhama makazi yao kwa sababu ya vitisho na utumiaji nguvu dhidi yao. Aila 2,000 za Wakristo hawo walihajiri makwao katika wakati huo. Thuluthi moja ya aila 1,000 kutokea vijiji vya wilaya ya Al Hamdaniya, mashariki ya mji wa Mosul wamesharejea majumbani mwao, kwa mujibu wa ripoti za UNHCR.

Toleo la karibuni la ripoti ya Shirika la UM juu ya Huduma za Utalii Duniani (UNWTO), taarifa inayotumiwa kama kipimahewa (baromita) kuhusu shughuli za utalii wa kimataifa, imethibitisha ya kuwa tangu kati ya mwaka 2008, kiwango cha utalii kimataifa kilianza kuteremka kwa kasi kabisa. Ripoti ya UNWTO inasema mzoroto huo unaashiria athari za kuongezeka kwa bei ya nishati kuporomoka kwa hali ya uchumi duniani, na vile vile kupwelewa kwa imani ya washtiri wa huduma hizo kimataifa.

Baraza Kuu linatazamiwa kufanyisha mkutano maalumu wa siku mbili katika Makao Makuu ya UM, utakaohudhuriwa na wawakilishi wote wa kimataifa, kuanzia Ijumatano ya tarehe 12 Novemba, ili kuzingatia maadili yanayotakikana kuimarisha kipamoja amani ulimwenguni. Mada ya mkutano huu, wa hadhi ya juu, inahimiza kuwepo “Utamaduni wa Amani kwa Wote”. Kwenye mazungumzo na waandishi habari adhuhuri ya leo Raisi wa Baraza Kuu, Miguel D’Escoto alibainisha kuwa na matumaini ya kutia moyo kutokana na mkusanyiko huo ambapo, alisema, viongozi na maofisa wakuu kutoka darzeni za mataifa watajaribu kuwafikiana juu ya hatua za kurahisisha na kuharakisha kipamoja utekelezaji wa mipango ya kukwamua vile vizingiti vinavyotatanisha mipango ya kimataifa yenye natija kwa wote, mathalan, kuondosha umaskini na kukomesha njaa duniani.