Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

~ Raisi wa Baraza Kuu la UM, Miguel D’Escoto aliwaambia wajumbe wa kimataifa waliohudhuria mkutano maalumu juu ya Utamaduni wa Amani kwamba ulimwengu unakabiliwa kwa sasa na kipindi kigumu kabisa ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu UM ulipobuniwa. Aliwahimiza wawakilishi wa Mataifa Wanachama kutumia “uzito walionao wa kimaadili” ya kiutu kusuluhisha matatizo thakili yalioambukiza Dunia yetu, mathalan, njaa, umaskini na athari haribifu za mabadiliko ya hali ya hewa. ~

Shirka la Mchanganyiko la UM/UA juu ya Ulinzi Amani kwa Darfur (UNAMID) limeripoti kuwasili leo, kwenye mji wa Nyala, Darfur Kusini wanajeshi 155 wa Misri, wakijumuisha maofisa 16 na askari 139. Wanajeshi hawa wanawakilisha Kombania ya Uchukuzi wa Vifaa Vizito na wanatarajiwa kujiunga na wenziwao saba waliowasili Darfur siku za nyuma. Wanajeshi wa Misri watashiriki kwenye operesheni za kugawa shehena za kukidhia mahitaji ya vikosi vya UNAMID vilioosambaa kwenye kambi mbalimbali kwenye jimbo la mgogoro, ikijumlisha mahitaji ya maji na nishati.

Mshauri wa UM juu ya Masuala ya Kijeshi, Jenerali Chikadibia Isaac Obiakor leo anazuru N’Djamena kushauriana na maofisa wa serikali pamoja na wale wa Shirika la Ulinzi Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad (MINURCAT). Mkutano wa Jenerali Obiakor na maofisa wa Chad utazingatia mfumo unaotakikana kuendeleza operesheni za UM baada ya vikosi vya Umoja wa Ulaya vya EUFOR kuondoka nchini mwezi Machi mwakani, vikosi ambavyo vilidhaminiwa kuhami na kuwahifadhi raia na wale wahamiaji waliopo Chad kaskazini-mashariki.

Benki Kuu ya Dunia imetangaza kutumia dola bilioni 100, katika miaka mitatu ijayo, ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kukuza uchumi. Tangazo hili limetolewa kabla ya mataifa wanachama wa kundi la G-20, kukusanyika mjini Washington D.C. kuhudhuria mkutano juu ya masuala ya uchumi wa kimataifa mnamo mwisho wa wiki, mkutano utakaofanyika katika mji wa Washington D.C. Kadhalika Benki Kuu ya Dunia imeahidi kuzipatia nchi maskini 78 misaada ya fedha ya muda mrefu, na pia misaada ya muda mfupi, pamoja na mikopo isio riba. Halkadhalika Benki ya Dunia imesema itaongeza msaada wake kwa sekta za binafsi napia kufadhilia mfuko wa hisa ya kimataifa itakayoziokoa zile benki zenye matatizo ya fedha.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu (UNFPA) limechapisha ripoti ya mwaka inayotathminia Hadhi ya Idadi ya Watu Duniani kwa 2008. Ripoti hiyo imepewa mada inayosema Kufikia Makubaliano ya Wote: Fungamano za Tamaduni, Jinsiya na Haki za Binadamu. Ripoti inatathminia uhusiano uliojiri baina ya tamaduni anuwai na haki za binadamu, hususan haki za wanawake. Ripoti imetilia mkazo juu ya umuhimu wa kutayarisha miradi itakayozingatia maadili halisi ya kitamaduni, kadhia ambayo inaaminiwa ndio yenye kuamua kama miradi ya maendeleo itakamilishwa na mafanikio au madhara. Ripoti imethibitisha mashirika ya kimataifa yanayohusika na miradi ya maendeleo, mara nyingi hayajali umuhimu wa kuzingatia maadili ya kitamaduni wanapotayarisha huduma za maendeleo, kitendo ambacho athari zake hudhuru uchumi kijumla.