Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM ameeleza, kwa kupitia msemaji wake, wasiwasi alionao juu ya kuendelea kuharibika kwa hali ya usalama na utulivu wa maisha kwenye Tarafa ya Ghaza na Israel kusini, na anakhofia maafa huenda yakapamba zaidi, yakichanganyika na vurugu kwenye eneo hilo. Amependekeza makundi yote husika kuhishimu haki za binadamu pamoja na kuthibitisha sheria za kimataifa juu ya hifadhi ya raia kwenye mazingira ya uhasama.~

Ofisi ya Mshauri Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati (UNSCO) imeripoti ya kuwa vituo vyote vya kuingilia Tarafa ya Ghaza vimefungwa kwa leo – ikijumlisha vile vivuko vinavyotumiwa kuingiza nishati na zile sehemu zinaotumiwa na wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kiutu na kihali kwenye eneo liliokaliwa kimabavu na Israel. Leo ni siku ya tisa mfululizo ambapo vikwazo vimelazimishwa na Israel dhidi ya ugawaji wa chakula kwa umma muhitaji katika Tarafa ya Ghaza, na vile vile dhidi ya shughuli zote za biashara. Ilivyokuwa mabomba yanayochukua nishati hayakuruhusiwa kupatiwa mafuta yanayohitajika kuendesha vinu vya taa, baadhi ya sehemu za Ghaza zitanyimwa umeme kwa muda wa saa 8 hadi 12 kila siku.

KM leo ameelekea mji mkuu wa Marekani wa Washington D.C. akijumuika na viongozi wa umoja wa kundi la G-20, ambao Ijumamosi wanatazamiwa kuhudhuria Mkutano Mkuu maalumu kujadilia namna ya kufufua uchumi uliozorota wa kimataifa, na pia kuzingatia taratibu za kurudisha utulivu wa bishara ya fedha kwenye soko la kimataifa. KM anatarajiwa kuwanasihi viongozi wa G-20 juu ya umuhimu wa kudhibiti kipamoja mzozo wa fedha ambao umetanda duniani sasa hivi, maana pakikosekana hatua hiyo, alihadharisha, madhara yake yatafumsha janga hatari la kimaisha kwa umma wa kimataifa katika siku zijazo.

Theresa A. Hitchens wa Marekani amechaguliwa na KM kama Mkurugenzi wa tano wa Taasisi ya UM juu ya Utafiti kuhusu Upunguzaji Silaha (UNIDIR). Anatazamiwa kuchukua madaraka haya mapya mjini Geneva katika mwezi Januari 2009 baada ya Patricia Lewis wa Uingereza kumaliza madaraka yake. Bi Hitchens hivi sasa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Habari za Ulinzi (CDI) kilichopo Washington D.C. kinachoshughulikia Miradi yaUsalama wa katika Anga.

UM umetangaza kwamba mapatano ya kusimamisha mapigano yanaendelea kuhishimiwa na makundi yanayohasimiana katika eneo la vurugu la Kivu Kaskazini, katika mashariki ya Jamhuri ya Kidemopkrasi ya Kongo (JKK) ijapokuwa hali, kwa ujumla bado ni ya kutia wasiwasi na isio na uhakika. Hali hiyo imeyawezesha mashirika yanayohudumia misaada ya kihali kuanza kugawa misaada ya kimsingi ya kunusuru maisha kwa umma ulioathirika na mzozo wa karibuni kwenye eneo hilo, mgogoro uliolazimisha robo ya watu milioni moja, kuanzia mwezi Agosti, kuhajiri makazi katika sehemu za mashariki ya nchi.