Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na mashirika wenzi waanzsiha huduma za afya kudhibiti kipindupindu katika JKK

WHO na mashirika wenzi waanzsiha huduma za afya kudhibiti kipindupindu katika JKK

Shirika la Afya Duniani (WHO) leo limechapisha taarifa rasmi yenye kusema ya kuwa tangu mwanzo wa mwezi Oktoba hadi mapema mwezi Novemba, katika eneo la Goma, ikijumlisha sehemu ya Karisimbi katika JKK, idadi ya watu walioambukizwa na magonjwa ya kipindupindu imeongezeka kwa mara tatu.

“Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na mashirika wenzi mengine ya kimataifa yameanzisha huduma za pamoja, kujaribu kudhibiti ongezeko la idadi ya wagonjwa walioambukizwa na maradhi ya kipindupindu, idadi ambayo imezidi mara tatu katika baadhi ya maeneo; mathalan, katika mji wa Goma, katika wiki ya kwanza ya Oktoba kulisajiliwa watu 44 waliopatwa na kipindupindu, na katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba watu walioambukizwa na kipindupindu ilikuwa sawa na 154. Hali hii imetokana na ukosefu wa utulivu na amani, pamoja na uhamaji wa idadi kubwa ya raia kutoka makwao kwa sababu ya mapigano, ikichanganyika na huduma dhaifu za afya kwenye eneo hilo, na vile vile kutokana na upungufu wa maji safi na usafi wa mazingira. Tunakhofia na kuashiria asilimia 30 ya wagonjwa hawa wa kipindupindu watafariki .. na juu ya yote hayo WHO pamoja na mashirika wenzi itaendelea kujitahidi kudhibiti mfumko huu wa kipindupindu, kwa uwezo wote walionao, na katika mazingira ya wasiwasi na vurugu. Hivi sasa tani 60 za madawa na vifaa vya afya zipo Kampala, Uganda zikisubiri kupelekwa Goma, na ni matumaini yetu kuanzia Ijumamosi malori matatu yatakayobeba tani 25 ya vifaa vya afya, vinavyofadhiliwa na WHO, yataanza safari ya kuelekea Goma kutokea Kampala, vifaa ambavyo vitawahudumia afya mamia elfu ya umma muhitaji, kwa kipindi cha mwezi mmoja mfululizo.”