Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limelaani vikali utenguzi wa karibuni wa maafikiano ya kusimamisha mapigano ulioharamishwa na kundi la waasi wa CNDP, walio wafuasi wa Jenerali Mtoro Laurent Nkunda. MONUC imeripoti helikopta zake zimeendeleza operesheni za upelelezi kwenye eneo la mapigano, na wanajeshi wa UM wamejiandaa kukabiliana na tukio lolote la dharura. Kadhalika MONUC imeyataka makundi yanayopigana kuhishimu ahadi yao ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuupatia mpango wa amani fursa ya mafanikio.~

Ijumaa na Ijumamosi iliopita KM Ban Ki-moon alikuwa mji mkuu wa Marekani wa Washington D.C. akihudhuria Mkutano Mkuu wa Kuzingatia Hali ya Uchumi wa Kimataifa. KM alisema anaunga mkono Taarifa ya Pamoja iliotolewa mwisho wa Mkutano ambapo viongozi wa kimataifa waliahidi kushauriana kuandaa vifurushi vya miradi kadha, itakayosaidia kufufua, kwa nguvu moja, uchumi wa ulimwengu, na kudhibiti bora utaratibu wa kuongoza shughuli za soko la kimataifa, kwa kujumuisha zaidi mataifa kwenye utawala wa uchumi huo, na kujaribu kujiepusha na sera ya kulinda biashara na uekezaji wa kizalendo dhidi ya waekezaji wa kigeni.

Ofisi ya Mshauri Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani Mashariki ya Kati (UNSCO) imeripoti Ijumatatu kufunguliwa, kwa muda, kivuko cha mpaka baina ya Israel na Tarafa ya Ghaza cha Kerem Shalom, uamuzi ambao uliliwezesha Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kupeleka malori tisa ya shehena ya chakula kitakachogaiwa umma muhitaji katika Ghaza. Lakini yale mabomba ya kuhamishia mafuta ya petroli bado ni matupu kwa sababu nishati imepigwa marufuku kupelekwa Tarafa ya Ghaza, ikimaanisha eneo hilila WaFalastina litaendelea kushuhudia matatizo ya umeme. Wakati huo huo, Shirika la Kufarajia Mahitaji na Huduma za Kihali kwa Wahamaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) yaliweza kupeleka malori manane Ghaza yaliochukua nyama na maziwa ya unga kwa watoto. Hata hivyo UNRWA imeripoti makontena ya maziwa yalifunguliwa kwa visu na wanajeshi wanaodhibiti mipaka wa Israel, tukio liliosababisha hasara kuu iliokadiriwa maelfu ya dola.

Taasisi Inayosimamia Mkataba juu ya Udhibiti wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) imetoa ripoti mpya inayodhihirisha kuzidi kwa kiwango cha gesi chafu inayomwagwa angani katika nchi zenye maendeleo ya viwandani. Ripoti ilisema kati ya miaka ya 2000 hadi 2007 yale mataifa 40 yaliowajibika kuripoti kwa Taasisi ya UNFCCC chini ya Mkataba wa Udhibiti wa Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa kuhusu namna yanavyodhibiti herwa chanfu angani, yamethibitisha kuongeza umwagaji wa hewa chafu angani kwa asilimia 2.3, na fungu kubwa la uharibifu huo ulijiri zaidi kwenye zile nchi zinazojaribu kurekibisha uchumi wao kwa kufuata mfumo wa soko huru, nchi ambazo uharibifu wa hewa chafu kwao uliongezeka kwa mara tatu zaidi. Mkurugenzi Mkuu wa UNFCCC, Yvo de Boer, alisema takwimu hizi zinaonyesha dhahiri ulazima wa kuchukuliwa maamuzi ya dharura, kwenye kikao kitakachofanyika Poznan, Poland wiki mbili zijazo ili kudhibiti mfumko huu.

Margareta Wahlstrom wa Uswidini ameteuliwa na KM kushika madaraka ya KM Msaidizi juu ya Upunguzaji wa Hatari ya Maafa, na pia kuwa Mjumbe Maalumu wa KM kwenye Makao Makuu ya Taasisi ya Miradi ya Kupunguza Maafa Kimataifa atakayesimamia utekelezaji wa Mfumo wa Hyogo kidharura. Wadhifa huu, unafadhiliwa na mchango wa khiyari, na ofisi inayohusika na miradi ya kusimamia udhibiti wa maafa ipo Geneva; na nafasi hii imebuniwa makhsusi kwa madhununi ya kuharakisha kwa vitendo, na ushirikiano wa kimataifa, majukumu ya kupunguza hatari ya maafa, ilivyokuwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinaoendelea kuongezeka ulimwenguni.