Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti kuhusu masuala ya kuongezwa majeshi katika JKK, mauaji ya mwanahabari na kushikwa kwa raia na vikosi vya serikali

Ripoti kuhusu masuala ya kuongezwa majeshi katika JKK, mauaji ya mwanahabari na kushikwa kwa raia na vikosi vya serikali

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK na Mkuu wa shirika la ulinzi amani nchini humo la MONUC, ametangaza masikitiko makuu kuhusu “mauaji ya kioga” ya Didace Namujimbo, mwanahabari wa Redio Okapi ambaye alipigwa risasi mnamo saa 9:30 Ijumamosi usiku, alipokuwa anarejea nyumbani Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.

Wanajeshi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Ijumapili waliwashika watu 25 kutoka msafara wa magari ya UM, watu ambao walidaiwa kuwa ni polisi wa serikali kutoka maeneo yalioshikwa na waasi. Kwa mujibu wa msemaji wa MONUC, Liuteni-Kanali Jean-Paul Dietrich, kati ya idadi hiyo walikuwemo waasi 10 waliojisalimisha kwa vikosi vya MONUC, shirika ambalo lilidhamiria Ijumatatu ya leo, kuwakabidhi waasi hawo, kwa jeshi la serikali. Alisema katika jumla hiyo walikuwemo pia polisi 10 wa serikali, pamoja na raia watatu.

Kadhalika, imeripotiwa na MONUC ya kwamba vikosi vyake vya walinzi amani kutoka Afrika Kusini, Bara Hindi, Pakistan na Uruguay vitapatiwa askari ziada, kufuatia azimio la tarehe 20 la Baraza la Usalama, lilioidhinisha kuongeza wanajeshi 3,100 ziada, kusaidia kudhibiti bora hali katika eneo la mtafaruku na vurugu, la mashariki katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Asilimia kubwa ya askari hawa wanatazamiwa kuenezwa na kudhibiti usalama katika Kivu Kaskazini na Kusini, ambapo waasi wenye jadi ya Kitutsi walifufua tena uhasama kuanzia mwezi Agosti.