Hapa na Pale

Hapa na Pale

John Holmes, KM Mdogo juu ya Masuala ya Kiutu na Mshauri wa UM Kuhusu Misaada ya Dharura Ijumanne ameanza ziara ya siku sita katika Sudan. Alizuru kambi ya Kalma, iliopo Nyala, Darfur Kusini yalipo makazi ya muda kwa wahamiaji wa ndani 88,000. Alipata fursa ya kuzungumza nawo na walimwomba wapatiwe hifadhi ziada kutoka vikosi mseto vya ulinzi amani vya UM na UA kwa Darfur, yaani vikosi vya UNAMID ambavyo polisi wake wanaendeleza doria ya kulinda kambi hizo kwa saa ishirini nanne mfululizo.

Juu ya utulivu kwenye eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) imethibitishwa na Shirika la UM linalosimamia huduma za amani (MONUC) kwamba hali huko inaendelea kuwa shwari, na bado hakujaripotiwa tukio kuu lilioharamisha maafikiano ya kusimamisha mapigano. Eneo jirani na Goma linaendelea kuwa ni la wasiwasi, na walinzi amani wa UM wanafanya doria mchana na usiku, hususan kwenye yale maeneo ambayo, hapo kabla, yalishuhudia vurugu na mapigano. Wakati huo huo Shirika linalohudumia Misaada kwa Wahamiaji (UNHCR) linajiandaa kuhamisha raia wahamiaji wa ndani, kutoka kambi za Kibati, na kuwapeleka maeneo salama, mbali na waasi na vikosi vya serikali. Uhamisho huu, ulio wa khiyari, utawalenga, awali, watu dhaifu pamoja na watoto wadogo, watu wagonjwa na wakongwe.

Ijumatatu alasiri, Mjumbe Maalumu wa KM juu ya mzozo wa mashariki katika JKK, yaani Raisi mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, alipokutana na waandishi habari katika Makao Makuu ya UM alisema mnamo mwisho wa wiki atarejea tena kwenye eneo la mgogoro, kuendeleza duru nyengine ya mazungumzo ya upatanishi na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa kundi la waasi wa CNDP na wadau wengien muhimu. Anatarajiwa kuwepo Kinshasa Ijumamosi, na kuelekea Goma Ijumapili, na vile vile kuzuru mataifa mengine jirani kwa mashauriano na viongozi kuhusu mpango wa amani.