Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama alasiri lilizingatia ripoti ya karibuni ya KM kuhusu maendeleo kwenye utekelezaji wa mapendekezo ya azimio 1701 katika Lebanon. Mratibu Maalumu wa UM kwa Lebanon, Michael Williams aliwapatia wajumbe wa Baraza taarifa yake kuhusu hali halisi Lebanon. Kadhalika Baraza la Usalama lilikuwa na mazungumzo ya hadhara kuhusu hali ya marekibisho Kosovo.

Asubuhi Baraza la Usalama lilisikiliza taarifa ya Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK). Doss alielezea ripoti ya karibuni ya KM kuhusu shughuli na operesheni za ulinzi amani katika JKK za MONUC. Ripoti ilisisitiza mzozo wa Kivu Kaskazini umeingia kwenye kipindi hatari, na inabashiriwa huenda kukazuka maafa makubwa ya kihali yatakayodhuru hali za umma raia, kwa ujumla. Doss alisema juhudi za kidiplomasiya, za kiwango cha juu kabisa, zimeshaanzishwa, kwa lengo la kusimamisha mapigano na kufufua utulivu na amani nchini. Aliongeza kusema vile vile ya kwamba ni muhimu kwa UM kuwa na uwezo unaoridhisha ili kujiandaa kuhami masilahi yake kwenye eneo la mtafaruku na vurugu, na kuhakikisha mapigano mapya hayatoanzishwa tena, hali ambayo anaamini itaruhusu mazungumzo ya amani kupata fursa ya kuendelea mbele, chini ya uongozi wa Mjumbe Maalumu wa Upatanishi wa KM, Olusegun Obasanjo.

Shiirika la Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limetoa taarifa yenye kulaani kile kinachodaiwa na wafuasi wa Jenerali mtoro Laurent Nkunda kuwa ni “operesheni za polisi kutuliza amani”, vitendo ambavyo vinatengua maafikiano ya kusitisha mapigano. Mapigano haya, kwa mujibu wa MONUC, yamejumlisha tabaka ziada la hali ya hatari kwa shughuli za kupeleka misaada ya kiutu kwa umma waathirika, ikichanganyika na mazingira ya uslama unaonedelea kuharibika. MONUC pia imeripoti mapambano yalitukia Ijumanne alasiri katika Kiwanja, baina ya waasi wa kundi la Nkunda na majeshi ya mgambo ya Mai-Mai. Athari hakika za mapigano haya bado hazijajulikana; lakini kinachoeleweka kihakika kwa sasa ni kwamba wakazi kadha wameonekana kuyahajiri mastakimu kwenye sehemu za mapigano na kuelekea mipakani Uganda.

Ofisi ya Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imeripoti kuanzisha, hivi sasa, kampeni ya siku 16 katika JKK, kuendeleza mafunzo maalumu ya kuwasaidia raia husika kutambua madhara na athari za vitendo haramu vinavyosababishwa na utumiaji mabavu wa kijinsiya, na kufahamisha taratibu za kufuatwa kukabiliana na suala hili, kwa usalama.

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) imeripoti kukamilisha warsha wa mafunzo maalumu Kinshasa, kwa mawakili raia wa JKK. Mafunzo haya yaliombwa na Serikali ya JKK yaendelezwe na UM kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kupamabana na ugaidi.

Baada ya Raisi Omar Al-Bashir kutia sahihi Ijumanne amri ya kuteua wawakilishi wa Kamisheni ya Kusimamia Uchaguzi wa Taifa, KM alitangaza kukikaribisha kitendo hicho kwa ridhaa, kitendo ambacho alisema ni muhimu katika maandalizi ya uchaguzi huru na wa haki mwakani, na kimewasilisha hatua muhimu kwenye utaratibu wa kuyatekeleza Mapatano ya Jumla ya Amani kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.

Ofisi ya Mratibu wa Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati (UNSCO) ameripoti leo kufunguliwa kwa kivuko cha Kerem Shalom, karibu na eneo liliokaliwa kimabavu la Tarafa ya Ghaza, na vile vile kufunguliwa kwa ukanda wa kusafirishia bidhaa wa Karni, pamoja na mabomba ya kuhamishia nishati ya Nahala Oz ambayo yalipatiwa lita wastani za nishati. Hatua hii iliochukuliwa na Israel imelipatia Shirika la UM juu ya Huduma za Kiutu kwa Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) fursa ya kupokea malori 12 yaliobeba bidhaa kadha za kiutu, zinazohitajika kunusuru maisha ya umma unaosumbuliwa na vikwazo vya kiuchumi dhidi yao katika Tarafa ya Ghaza. Bidhaa hizi zilijumlisha mchele na mafuta ya kupikia, pamoja na msaada wa madawa na chakula kutoka Serikali ya Jordan. Licha ya Mji wa Ghaza kuwa ilibahatika kufadhiliwa nishati wastani, wakazi wa eneo hilo bado wanaendelea kushuhudia matatizo ya umeme ambao huzimwa kwa masaa kadhaa kila siku. Mratibu wa Misaada ya Kiutu kwa maeneo yaliokaliwa kimabavu ya Wafalastina, MaxwellGaylard alipokuwa anaanzisha kampeni ya maombi ya kufadhiliwa mchango wa kimataifa kuhudumia kihali umma wa KiFalastina, kwenye mji wa Jerusalem hii leo, alisema kwamba hali katika maeneo hayo ni sawa na “mashambulizi na uvamizi unaovunja kihakika hadhi ya kiutu.” Aliongeza kusema idadi kubwa ya WaFalastina, hususan wale wakazi wa Tarafa ya Ghaza, wanaelemewa na mzigo mkubwa kimaisha, ambapo hulazimika kila siku kupambana na matatizo na shida za kupata chakula, maji ya kukidhi mahitaji ya chakula na kuoshea watoto wao.