Mkuu wa IAEA asema shirika limefikia "Njia Panda" kikazi, lahitaji misaada maridhawa kuendesha shughuli zake

Mkuu wa IAEA asema shirika limefikia "Njia Panda" kikazi, lahitaji misaada maridhawa kuendesha shughuli zake

Ijumatatu, tarehe 29 Septemba (08) Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) lilianzisha rasmi mkutano wa mwaka, uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka Mataifa Wanachama 145. Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Mohamed ElBaradei alisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi, na ninamnukuu hapa, “hali ya kazi katika IAEA hairidhishi na sio nzuri.”

ElBaradei alikumbusha, jumuiya ya kimataifa imefikia “njia panda” hivi sasa na kunahitajika kufanyika marekibisho ya haraka ili kulisaidia Shirika la IAEA kupata uwezo unaofaa, wa kuimarisha huduma zake kama inavyotakikwa. Alisema upungufu wa fedha za kuendesha kazi za IAEA umedhoofisha miundombinu yake, hali ambayo imelifanya shirika kutegemea zaidi michango ya dharura kutoka nchi wanachama kuweza kuhudumia shughuli muhimu, msaada ambao mara nyingi huunganishwa na masharti mbalimbali yenye kuzorotisha kazi. Kwa mfano, alisema, asilimia 90 ya mradi wa IAEA unaohusika na usalama wa huduma za nyuklia duniani, mradi ambao lengo lake moja muhimu hasa ni kuwanyima magaidi fursa ya kumiliki vifaa vya kinyuklia, mradi huu hutegemea zaidi michango ya khiyari kutoka wahisani wa kimataifa.

Vile vile El Baradei alisema moja ya tatizo sugu ambalo bado linaikabili IAEA kwa sasa ni lile linalohusu viwanda vya nishati ya nyuklia vya Iran. Alikiri kwamba maendeleo makubwa yalishapatikana kuthibitisha masuala kadha juu ya mradi wa viwanda vya nishati ya nyuklia katika Iran, hasa zile taarifa zinazohusu mradi wa kusafisha yuraniamu halisi inayotumiwa kutengenezea nishati ya umeme. Alisisitiza kwenye risala yake kwamba hakuna mbinu zozote za kuashiria kwamba Iran inatumia mradi huo kwa shughuli zilizokwenda kinyume na matamko yao. Hata hivyo, aliendelea kusema, IAEA haiwezi kuthibitisha kihakika kama hakuna zana za kinyuklia zisiotangazwa wala shughuli za kijeshi za kinyuklia ziliofichwa. Alikumbusha kwamba ijapokuwa Iran ilishiriki kwenye shughuli za kusafisha kiasi kidogo cha madini ya yuraniamu, shughuli ambazo zinasimamiwa na IAEA, baadhi ya wanachama wa jumuiya ya kimataifa bado hawajaridhika na ukaguzi wa IAEA na wana wasiwasi kuhusu dhamira hasa za mradi wa nishati ya nyuklia wa Iran kwa sababu, alisema, ya ukosefu wa uwazi kamili wa miradi iliopita na ile miradi mipya ya nyuklia ya Iran, wasiwasi ambao ulibainika kwenye kikao cha karibuni cha Bodi la Magavana wa IAEA, na kujumuishwa kwenye maazimio kadha yaliopitishwa na Baraza la Usalama.

Kutokana na hali hiyo El Baradei aliiomba Iran ijitahidi kutekeleza pendekezo la kuruhusu ukaguzi zaidi wa miradi yake ya nyuklia, na kujenga hali ya kuaminiana kimataifa, mapema iwezekanavyo, ili kuthibitisha kihakika kwamba miradi ya viwanda vyake vya nyuklia nchini itatumiwa kuzalisha nishati ya umeme kwa raia pekee na sio kwenye huduma za kijeshi. Mwelekeo huu ukitekelezwa, alimaliza kisema, El Baradei utawasilisha mazingira mazuri ya kuaminiana, na itakuwa jambo zuri sana kwa Iran, kwa eneo la Mashariki ya Kati na kwa ulimwengu mzima.

Vile vile Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, aliyakumbusha Mataifa Wanachama kwamba kila taifa mwanachama lina haki ya kanzisha viwanda vya nishati ya nyuklia kukuza maendeleo, hasa katika nchi maskini, chini ya uangalizi na usimamizi wa IAEA. Alisema katika miaka miwili iliopia karibu nchi 50 zilishaonyesha upendeleo wa kuanzisha nishati ya umeme inayotokana na nguvu za nyuklia na kuomba IAEA iwasaidie, kama anavyoelezea hapa:

El Baradei alimaliza kwa kudhihirisha kwamba sasa hivi nchi 12 zinajiandaa kikamilifu kuanzisha viwanda mpya vya nguvu nyuklia kuhudumia umeme. Alikiri kwamba IAEA si shirika pekee lenye ujuzi kuhusu matumizi ya nishati ya kinyuklia, lakini pia alikumbusha ukweli ulivyo ni kwamba nchi nyingi zinaamini ushauri wa IAEA usiopendelea unahitajika, na ni muhimu katika kusimamia shughuli za matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Sikiliza habari kamili kwenye idhaa ya mtandao.