Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alain Le Roy, Naibu KM mpya wa Idara yaUM kuhusu Operesheni za Ulinzi Amani Duniani (DPKO) amewasili Sudan Ijumatatu asubuhi, kwa ziara ya wiki moja. Dhamira ya ziara hii ni kujijulisha na kukutana kwa mashauriano na viongozi wa Serikali ya Muungano wa Taifa na Serikali ya Sudan Kusini, pamoja na washiriki wengine wa huduma za amani wa eneo hilo la Afrika. Kadhalika Le Roy anatazamiwa kukutana na wakuu wa mashirika ya amani ya UM katika Sudan ya UNMIS, na wakuu wa vikosi vya amani vya mchanganyiko vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa Darfur, UNAMID. Le Roy alianza madaraka mapya ya khatamu za kuendesha Idara ya DPKO mwezi Agosti mwaka huu.

Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limewakilisha ripoti mpya kuhusu maendeleo ya miaka mitano katika utekelezaji wa mapendekezo ya kuimarisha elimu ya Mwongo wa UM wa Ujuzi wa Kusoma na Kuandika (2003-2012). Ripoti ilisema ujuzi wa kusoma na kuandika uliongezeka katika mataifa yanayoendelea kuanzia 2003 hadi kipindi cha sasa hivi, juu ya kuwa misaada ya fedha ilikuwa haba kutosheleza kadhia hiyo kama inavyotakikana. Kwa hivyo, kiwango cha ujuzi wa kusoma na kuandika kinatarajiwa kufikia asilimia 87 katika 2015 kutokana na hatua zinazochukuliwa kimataifa kwa sasa, ambazo lengo lake lilikuwa ni kupunguza kwa nusu kima cha kupambana na ujinga.

Mkutano wa Dunia wa Nne juu ya Watoto Waathiriwa wa UKIMWI/VVU umeanza rasmi Ijumatatu kwenye mji wa Dublin, Ireland ambapo kulitolewa mwito uyatakayo mataifa tajiri kufadhilia mafurushi ya misaada ya huduma za kijamii kwa nchi zinazoendelea, ili ziweze kukabiliana vyema na matatizo ya ufukara wa watoto, na pia kuzisaidia kihali zile kaya zilizoteseka zaidi na maradhi hayo.