Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) limeripoti Alkhamisi kuwa Jamhuri ya Kideokrasi ya Umma wa Korea (DPRK), ambayo pia hujulikana kama Korea ya Kaskazini, imearifu rasmi kwamba wataalamu wa IAEA hawaruhusiwi tena kukagua viwanda vya kinyuklia viliopo Yongbyon kuanzia hivi sasa. Kadhalika DPRK imearifu kwamba imesitisha zile shughuli za kulemaza huduma za kinyuklia katika Yongbyon, shughuli ambazo zitafufuliwa tena karibuni, kinyume na yale makubaliano yaliofikiwa baada ya Mazungumzo ya Pande Sita. Shirika la IAEA limesema litasalia Yongbyon kusibiri taarifa ziada kutoka Serikali ya DPRK.

Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio la kuongeza kwa miezi minne ziada Operesheni za Uangalizi za UM katika Georgia zinazoongozwa na Shirika la UNOMIG. Uamuzi huu ulichukuliwa baada ya mashauriano ya kwenye Baraza la Usalama na Mjumbe Maalumu wa KM kwa Georgia pamoja na Edmond Mulet, KM Mdogo anayehusika na Operesheni za Ulinzi Amani za UM katika ulimwengu. Kadhalika Barazala Usalama, kwenye kikao cha faragha, lilisikia ripoti kuhusu maendeleo na kazi za Kamati juu ya Vikwazo Dhidi ya Usomali, inayoongozwa na Balozi Dumisani Kumalo wa Afrika Kusini.