Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) imeripoti hali ya chakula Ethiopia inaendelea kuharibika. Kwa mujibu wamakadirio ya laribuni ya Serikali ya Ethiopia na washiriki wenzi wa huduma za kiutu watu milioni 6.4 wanahitajia kufadhiliwa misaada ya dharura ya chakula kwa sasa angalau kunusuru maisha. Huo ni muongezeko wa asilimia 40 tangu Juni 2008. Kwa sababu hiyo, watu wingi zaidi wanahamia mijini kutafuta chakula kutokea vijijini. Vitovu vitatu vya ugawaji chakula kwa umma muhitaji vinatayarishwa kwa sasa kuwapatia posho inayofaa karibu watu milioni mbili muhitaji wanaoishi kwenye eneo husika. Mashirika ya UM ya WHO na UNICEF nayo pia yamejumuisha mchango wao kudhibiti miripuko ya magonjwa ya kuambukiza.

Shirika la Kimataifa juu ya Uhamiaji (IOM) limeripoti walimu 15 waliohitimu taaluma ya ilimu na waliokuwa wakiishi kwenye kambi za wahamiaji wa ndani mjini Khartoum wameamua kurejea Sudan Kusini kuanza kazi. Walimu hao na aila zao, wakifuatana na watumishi wa IOM, walitumia usafiri wa barabara kupitia miji ya Kosti na Kadugli, na walitarajiwa Wilaya ya Pariang Ijumaa. Walimu hawa ni miongoni mwa kundi la walimu 264 waliofadhiliwa msaada wa Ujapani na Denmark uliokusudiwa kuziba pengo hatari la upungufu wa taaluma na ujuzi wa kiufundi unaotakikana kukidhiwa kimataifa, kama ilivyotathminiwa na Serikali ya Sudan Kusini, hususana katika sekta za ilimu na afya.

Tarehe 10 Oktoba ndio tarehe sahihi ya Siku ya Kuhamasisha Uangalizi Bora wa Magonjwa ya Akili Duniani – na sio tarehe 09 Oktoba, kama ilivyoripotiwa kwenye taarifa ya Alkhamisi. Kwenye risala aliowasilisha KM kuiadhimisha siku hiyo alikumbusha tena ya kwamba miradi ya afya pote ulimwenguni inakabiliwa na jukumu adhimu la kuhudumia haraka matunzo ya afya ya akili, na hifadhi inayofaa kuimarisha haki za binadamu kwa wale watu wanaougua sana ugonjwa wa akili. Thoraya Obeid, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) alisema kwenye risala yake kuihishimu Siku ya Kuhamasisha Uangalizi wa Magonjwa ya Akili Kimataifa tusisahau umuhimu wa kuwapatia mama wazazi tiba bora ya maradhi haya. Alisisitiza kwamba anapoathirika mama mzazi mtoto naye pia huumia na hata huhatarishwa kimaisha. UNFPA na Shirika la Afya Duniani (WHO) yamejumuika kuunganisha miradi inayohusu huduma za uzazi bora na sera za afya ya mtoto pamoja na masuala yanayohusu utimamu wa akili.