'Msiba mwengine wazuka Ghuba ya Aden': UNHCR

10 Oktoba 2008

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa imejumuika na washiriki wengine wa kimataifa kuwatafuta wahamiaji karibu 100 wanaoripotiwa kupotea katika Ghuba ya Aden, baada ya kulazimishwa na wafanya magendo kuchupa kutoka kwenye chombo walichokuwemo, nje ya mwambao wa Yemen.

"Kumetukia msiba mwengine katika Ghuba ya Aden, na UNHCR pamoja na washiriki wengine wanajitahidi kuwatafuta wahamiaji wanaokadiriwa 100 walioripotiwa wamepotea kwenye Ghuba ya Aden, baada ya kulazimishwa na wafanyamagendo kuruka majini kutoka kwenye mashua waliokuwemo, nje ya mwambao wa Yemen. Baadhi ya watu 47 walionusurika na ajali hiyo waliwaarifu watumishi wa UNHCR katika Yemen kwamba Ijumatatu mashua iliochukua watu 150 (mia moja na khamsini) iliondoka kutoka bandari ya Usomali ya Marera, karibu na Bosaso na kwa muda wa siku tatu ilipwelewa baharini ikijaribu kuvuka ghuba kuelekea Yemen. Walipowasili kwenye eneo liliopo kilomita tano kutoka mwambao wa Yemen abiria wote, isipokuwa watu 12, walilazimishwa kuruka majini. Abiria hao 12 waliosalia waliteremshwa kwenye mashua ndogo wakati abiria waliochupa majini walimalizikia kupambana na mawimbi wakijaribu kuogelea kuelekea nchi kavu."

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter