Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama leo asubuhi limesailia ripoti iliowasilishwa na Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Kai Eide kuhusu shughuli za Ofisi ya Ujumbe wa UM Inyosaidia Ujenzi wa Amani Afghanistan (UNAMA). Eide aliwaarifu wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba katika miezi michache iliopita hali Afghanistan iliendelea kuharibika, hususan katika miezi ya Julai na Agosti ambapo idadi ya matukio yaliohatarisha usalama ndani ya nchi ililingana, kwa marudio, na ile hali ya hatari kuu iliojiri katika 2002. Kadhalika, Ijumanne Baraza la Usalama limpitisha, kwa kauli moja, azimio la kuongeza kwa miezi 12 zaidi shughuli za Shirika la Kusawazisha Utulivu na Amani Haiti (MINUSTAH) na zitaendelea hadi tarehe 15 Oktoba 2009.

Ofisi ya UNHCR imetoa ombi la dharura linaloihimiza jumuiya ya kimataifa kuwapati makazi wale wahamiaji waliokuwa wakiishi Iraq na ambao wamekwama kwa miaka miwili kwenye kambi za muda zilizotanda mipakani kati ya Iraq na Syria. UNHCR inasema hali ya maisha kwenye mazingira haya ni ngumu na ya shida sana, ambapo qwahamiaji hukabiliwa na joto kali sana, dhorubaza mara kwa mara za michanga, usalama dhaifu, majai machafu yaliotwama nje karibu na mahema pamoja na mwahali pa kupikia, mazingira ambayo vile vile yamekosa huduma za matibabu na ukosefu wa hata magari ya wagonjwa.

Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeripoti mataifa 20 yameidhinisha hivi sasa Mkataba wa Kuhifadhi Urithi wa Kitamaduni Ulimwenguni Uliopo Chini ya Bahari. Mkataba huu utafanywa kuwa sheria tarehe 02 Januari 2009. Mkutano Mkuu wa UNESCO ulipitisha azimio la kuwa na chombo hiki cha kisheria 2001, kwa makusudio ya kuhifadhi urithi tajiri wa utamaduni huo: ikijumlisha meli ziliyozama majini, mandhari asilia, sanaa za uchoraji za kwenye majabali ya mapangoni na yale magofu yaliopo majini. Mkataba unawakilisha mchango wa jumuiya ya kimataifa katika kupambana na tatizo la kuongezeka kwa wizi na uharibifu wa urithi wa utamaduni uliopo chini ya bahari.

Ofisi ya OCHA inasema mapigano na ujambazi ni hali iliosababisha idadi kubwa ya watu kung’olewa makwao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, zaidi katika sehemu ya Kaskazini, jumla ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu 2006. Watu 100,000 walisajiliwa kuomba hifadhi katika mataifa jirani ya Cameroon, Chad na Sudan licha ya kuwa mataifa mawili kati yao nayo pia yanakabiliwa na hali ya vurugu pamoja na usalama dhaifu.