'Watu 50,000 wamelazimika kuhajiri mastakimu katika JKK’: UNHCR
Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti makumi elfu ya wakazi wa jimbo la Ituri, kaskazini-mashariki ya JKK wamelazimika karibuni kuhama mastakimu yao kutokana na mapigano makali baina ya vikosi vya Serikali na waasi wa Uganda wa kundi la LRA.
Kwa mujibu wa makisio ya hivi sasa zaidi ya watu 50,000 walilazimika kuhama nyumba zao katika jimbo la Ituri, kaskazini-mashariki ya JKK kwa sababu ya mapigano makali baina ya maejshi ya Kongo na waasi wa Uganda wa kundi la LRA.” Alisema mapigano haya yalianza mwezi Septemba, na watu wingi walishapoteza maisha, kwa mujibu wa ripoti za watumishi wa UNHCR katika eneo hilo, pamoja na ushahidi uliokusanywa kutokana na wahamiaji waliong’olewa makazi na pia taarifa za watawala wa mahala hapo. Waasi wa LRA waliripotiwa waliharibu nyumba za watu, kwa kisasi, na hata kuangamiza majengo ya raia, halkadhalika. Watawala wa kienyeji walithibitisha raia karibu 100 walionekana wakielea kwenye mto baada ya kuuliwa na waasi wa LRA. Kadhalika, katika kipindi hicho hicho watoto 80 inaripotiwa walipotea. Wazee wa watoto hawa wanakhofia watoto wao walitoroshwa na waasi wa LRA ambao huwatumia kwenye mapigano.