Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK na Shirika la MONUC wameelezea wahka wao mkuu juu ya namna ya kuwahifadhi wale raia walio dhaifu kihali katika Kivu Kaskazini, kufuatilia mapigano yaliopamba katika wiki za karibuni. Mamia elfu ya raia katika Kivu Kaskazini wamelazimika kuhama makwao na kuelekea kwenye kambi za wanajeshi wa UM kupata hifadhi na mahali pa himaya. Hivi sasa vikosi vya ulinzi amani vya UM vimelazimika kugawana posho yao ya chakula na akina mama na watoto 400 waliohamia kambini mwao kutafuta ulinzi. MONUC pia inatathminia utaratibu unaofaa kuendeleza operesheni zake kwa sababu ya kufumka uadui dhidi ya vikosi vya UM katika Kivu Kaskazini na kwengineko nchini. MONUC ilibainisha watumishi wa UM kila siku hukabiliwa na hali ambayo, kwanza, huwalazimisha kujihami wao wenyewe kutokana na ghadhabu na uhasama dhidi yao ya raia, kabla hawajawasaidia umma dhaifu kwenye eneo la machafuko na vurugu.

Ijumatano alasiri Baraza la Usalama limepitisha, bila kupingwa, azimio la kuongeza kwa mwaka mmoja zaidi madaraka ya Kundi la Wataalamu wanaohusika na suala la Sudan, mpaka tarehe 15 Oktoba 2009. Kadhalika Baraza la Usalama limeidhinisha Taarifa ya Mwenyekiti iliokaribisha hatua ya Guinea-Bissau kuahidi kufanyisha uchaguzi wa bunge katika Novemba 16. Taarifa hiyo vile vile ilitoa mwito kwa Serikali Guinea-Bissau na wahusika wote kuhakikisha mazingira ya uchaguzi nchini yatakuwa na uwazi unaoaminika, na uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Taarifa ya Baraza la Usalama iliongeza kusema wajumbe wake wana wasiwasi mkuu juu ya kuongezeka kwa biashara haramu ya madawa ya kulevya na uhalifu wa mipangilio nchini unaohatarisha usalama na amani ya Guinea-Bissau.

Shirika la UM Kuhusu Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limependekeza kuchukuliwe hatua za haraka kimataifa kusaidia Zimbabwe kukabiliana na matatizo yaliovaa mfumo wa elimu nchini, utaratibu ambao UNICEF unausifu kuwa miongoni mwa taratibu bora kabisa za elimu barani Afrika. Iliripotiwa mfumo wa elimu Zimbabwe sasa hivi umeharibika kwa sababu ya mchanganyiko wa matatizo ya walimu kulipwa mishahara midogo, mahudhurio dhaifu kati ya walimu na wanafunzi pamoja na shida za usafiri na uhaba wa chakula, halkadhalika.

Imeripotiwa na wataalamu wa kimataifa ya kwamba gesi ya asidi kaboniki inayofonzwa baharini imegundulikana kuongezeka kwa kiwango kikubwa sana karibuni, kitendo ambacho kinahatarisha mfumo wa ikolojia na pia kuhatarisha makumi milioni ya watu wanaotegemea ajira kutoka baharini. Matokeo haya yaliripotiwa kwenye mkutano uliomalizika karibuni Monaco ulioandaliwa na washiriki kadhaa, ikijumlisha Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Shirika la Kimataifa juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Kinyuklia (IAEA). Wajumbe walioshiriki mkutanoni wameafikiana kwamba upunguzaji wa hewa chafu kwenye anga ndio njia madhubuti inayoweza kupunguza uharibifu unaoletwa na gesi ya asidi ya kaboniki baharini, kadhia ambayo ilisisitizwa inamudika na inaweza kufikiwa.

Alkhamisi (16/10/2008) Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi wa Kimataifa (ILO) limetoa ripoti mpya kuhusu Tofauti ya Mapato katika dunia. Kwa mujibu wa ILO, tofauti za mapato ya kibinafsi zimeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi katika sehemu nyingi za ulimwengu, hali ambayo vile vile inabashiriwa kukithiri zaidi sasa hivi, kwa sababu ya mzozo wa fedha uliozagaa kwenye soko la kimataifa. Yote haya yanatokea kwenye kipindi ambapo kumeshuhudiwa ukuaji wa uchumi wa nguvu uliozalisha milioni ya vibarua na kazi, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1990.