Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon amelaumu mauaji ya wahudumia wawili wa misaada ya kiutu, mmoja katika katika Usomali na mwengine katika Afghanistan, yaliotukia siku tatu zilizopita. Amewatumia mkono wa taazia aila, marafiki pamoja na wafanyakazi wenzi na amesema amechukizwa na matumizi ya nguvu, kwa makusudi, dhidi ya wale wanaoongoza kila juhudi za kuwapunguzia maumivu makubwa ya kimaisha kwa umma wa Afghanistan na nchini Usomali. Alisema alishtushwa na kuongezeka kwa mauaji na utoroshaji wa wahudumia misaada ya maendeleo katika mataifa hayo mawili. Aliwataka makundi yote husika kuheshimu hadhi isiofungamana na upande wowote, na isiopendelea, ya wafanyaklazi wanohudumiamisaaada ya kiutu, na kuwaruhusu waendeleze shughuli zao zenye dhamira ya kusaidia kunusuru maisha kwa mamilioni ya Wasomali na Waafghani wanaotegemea kufadhiliwa posho hiyo kuishi.~

Kundi la kwanza la maofisa wa polisi kutokea Nepal wamewasili Nyala, Sudan ambapo wanatarajiwa kuendeleza operesheni za mbinu maalumu za kudhibiti fujo za umati, wakiwa miongoni mwa vikosi vya Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa Darfur (UNAMID) vinavyohitajika kuimarisha amani kwenye eneo hilo la Sudan magharaibi. Wenziwao 147 ziada wanatazamiwa kuwasili nchini baadaye katika wiki. Vikosi vya Polisi vya Nepal ni kundi la tatu kuwasili Darfur kujiunganisha na Shirika la Ulinzi Amani la UNAMID, kufuatilia vikosi vya polisi kutoka Bangladesh na Indonesia. UNAMID inatarajia jumla ya vikosi vya polisi kutoka mataifa 19 wanachama kusimamia operesheni za amani katika Darfur.

Juan Somavia, aliye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) leo amewasilisha taarifa mpya juu ya ajira kwenye mazingira yaliopambwa na mzozo wa fedha. Alitahadharisha watu milioni 20 ulimwenguni watanyimwa kazi kwa sababu ya mgogoro wa fedha ulimwenguni. Alibainisha ya kuwa mnamo 2007 jumla ya watu waliokosa kazi ilikuwa sawa na milioni 190, idadi ambayo inashiriwa kufikia milioni 210 katika 2009. Vile vile Somavia alisema wafanyakazi maskini wenye pato la chini ya dola moja kwa siku, nayo pia inatazamiwa kuongezeka kwa jumla ya wafanyakazi milioni 40 kimataifa. Alikhofia mzozo wa fedha uliojiri kwa sasa duniani utaathiri zaidi sekta zinazoambatana na ujenzi, viwanda vya kutengenezea magari, sekta za utalii, fedha, biashara ya kutoa huduma na pia mali halisi isiyohamishika ya makazi.