Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Kenya yahitajia misaada ya kimataifa, inasema OCHA

Mafuriko Kenya yahitajia misaada ya kimataifa, inasema OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba nchini Kenya, katika wilaya ya Mandera, mvua kali zilizonyesha huko karibuni zilisababisha ukingo wa mto kubomoka na kuzusha mafuriko yalioathiri zaidi ya kaya 1,000.

"Mafuriko yamezuka nchini Kenya karibuni, hasa kwenye maeneo ya kaskazini-mashariki na kaskazini magharibi. Kwenye wilaya ya Mandera, iliopo kaskazini-mashariki watu 6,000 inaripotiwa waling’olewa makwao na kuathiriwa na mafuriko, na watu watatu walifariki, na jumla ya watu 16 imesajiliwa walipotea hivi sasa. Mafuriko haya yalifumka baada ya mvua kali kunyesha kieneo kuanzia tarehe 16 Oktoba, mvua ambazo ziliasababisha ukingo wa Mto Dawa kubomoka. Skuli katika wilaya ya Mandera kwa sasa zimefungwa kwa sababu ya mafuriko. Kilomita moja ya eneo linalotumiwa kuchota na kugawia maji nalo limeharibiwa kikamilifu, na kuna hatari ya uchafuzi na sibiko la maji hayo, kwa sababu vyoo katika eneo hilo navyo pia vimefurika maji; na hali hii tuseme kama haijadhibitiwa mapema huenda ikafumsha maradhi yanayochochewa na maji machafu na kuhatarisha afya kwa wakazi 150,000 wa eneo hilo."