Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama lilikutana Alkhamisi asubuhi kuzungumzia hali ya amani na usalama katika bara la Afrika. Wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kumsikiliza Raisi Ismail Omar Guelleh wa Djbouti akizungumzia kuzuka kwa hali ya wasiwasi, na mvutano hivi karibuni, baina ya taifa lake na nchi jirani ya Eritrea. Mwakilishi wa Eritrea, Araya Desta pia alihutubia Baraza la Usalama baadaye. Mkutano wa leo wa Baraza la Usalama uliadhimisha kikao cha 6,000 cha taasisi hii ya UM.~

Wanajeshi 163 wa Bangladesh wenye kuwakilisha Vikosi vya Majukumu Mengi ya Ugavi na Usafirishaji wa Watu na Vitu leo wamewasili kwenye mji wa Nyala, Darfur Kusini ambapo watasaidia pakubwa vikosi vya mchanganyiko vya kulinda amani Darfur vya UM/UA (UNAMID) kuendeleza kazi zake kwa urahisi,kama ilivyopendekezwa na jumuiya ya kiamataifa. UNAMID imeripoti maofisa waliosalia 162 kutoka Bangladesh wanatazamiwa kuwasili Darfur Ijumaa.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti watu zaidi ya 35,000 waling’olewa makazi katika mji wa Mogadishu mnamo mwezi Septemba, ikijumlisha watu milioni moja waliolazimika kuhajiri makwao na kumalizkia kuwa wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs). OCHA inasema wimbi hili jipya la wahajiri wa ndani lilizushwa na mapigano baina ya vikosi vya Serikali, vikisaidiwa na majeshi ya Ethiopia na vikosi vya Umoja wa Afrika vya UNISOM dhidi ya makundi kadha ya majeshi ya mgambo. Licha ya kuwa hali nchini Usomali ni mbaya kutokana na vurugu, ikichanganyika na ukame sugu, hata hivyo Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na washiriki wanaowakilisha mashirika yasio ya kiserikali wameweza katika wiki za karibuni kuwapelekea chakula watu milionimbili muhitaji nchini.

Mashirika ya UM yamependekleza yafadhiliwe msaada wa dola milioni 30 unaohitajika kuwahudumia kihali waathiriwa wa vimbunga vinne vilivyopiga Cuba kati ya miezi ya Agostu hadi Septemba mwaka huu, maafa ambayo yaliangamiza mamia elfu ya majengo na kuharibu miundombinu katika nchi.

John Homes, Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura ameanza ziara rasmi Haiti kutathminia mahitaji ya kitaifa kutokana na uharibifu ulioletwa na vimbunga vikali vilivyogharikisha nchi wakati wa majira ya tofani. Hali hii imerudisha nyuma sana huduma za kimataifa za kukomesha hali duni katika Haiti. Kwa mujibu wa OCHA jamii ya kimataifa iliahidi kuchangisha dola milioni 106 kuisaidia Haiti kukabiliana na maafa ya vimbunga, na kati ya jumla hiyo ni dola milioni 24.8 tu zilizopokelewa na UM na mashirika yake. Holmes anatarajiwa kushauriana na wakuu wa serikali kuhusu taratibu bora za kukidhi mahitaji ya kiutu kwa raia waathiriwa, na atatathminia nawo maandalizi yanayofaa kitaifa kukabiliana na maafa ya kimaumbile.

Martin Scheinin, Mkariri/Mtaalamu Huru wa UM juu ya ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu katika mazingira ya kukabiliana na ugaidi aliiambia Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu – ambayo inahusika na masuala ya kijamii, kiutu na kitamaduni – kwamba mfumo wa Marekani wa kutumia tume za kijeshi kuhukumu watu waliotuhumiwa ugaidi, waliopo kizuizini kwenye Ghuba ya Guantanamo, ni mfumo unaotengua kanuni za kimataifa dhidi ya uendeshaji kesi wa haki. Alisema fafanuzi hizi alizithibitisha zaidi baada ya kuzuru vituo vya kufungiwa watu waliotuhumiwa ugaidi vya Ghuba ya Guantanamo mwezi Disemba 2007 juu ya uharamu wa tume hizo za kijeshi kuhukumu raia.

Kwenye mahojiano na Kituo cha Habari cha UM, Asma Jahangir, Mkariri/Mtaalamu Maalumu juu ya uhuru wa itikadi na dini amedhihirisha wafuasi walio wachache kidini wanaendelea kubaguliwa katika sehemu kadha wa kadha za kimataifa kwa sababu ya itikadi zao, na mara nyingi hukabiliwa na “vitisho vinavyoendelezwa kwa muda mrefu” dhidi yao. Alisema asilimia kubwa ya walio wachache kidini huteswa zaidi kwenye yale mataifa yenye utawala wa kidhalimu na udikteta. Alitahadharisha ya kwamba uharamishaji wa haki ya kimsingi ya kuwa na itikadi na dini hujiri kwenye mataifa yenye mifumo mbalimbali ya kisiasa. Miongoni mwa ubaguzi alioshuhudia kwenye safari zake, aliongeza kusema, ni ile tabia ya kutoruhusu wafuasi wa dini ya wachache kukusanyika pamoja kufanya ibada ya jamaa, mara nyengine zile sehemu wanazofanyia hunajisiwa kwa makusudi, na hata hunyimwa ruhusa ya kuhiji. Bi Jahangir pia alipata fursa ya kuwasilisha fafanuzi hizo mbele ya ile Kamati ya Tatu inayohusu masuala ya kijamii, kiutu na kitamaduni hapo jana.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetangaza kwamba linawasaidia mamia ya Wakristo wa Iraq waliohama makwao kutoka mji wa kaskazini wa Mosul na kuelekea kwenye taifa jirani la Syria, taifa ambalo vile vile ni mwenyeji kwa wahamiaji milioni 1.2 wa Iraq waliohajiri makwao baada ya vurugu kuzuka nchini katika miaka ya karibuni. UNHCR imeripoti katika wiki za karibuni maelfu ya Wakkristo wa Iraq walihama Mosul na wingi wao walisalia kwenye jimbo la Ninawa, Iraq na kati ya hawo wahamiaji 400 walielekea Syria.