Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Charles Vincent, Mkurugenzi wa Ofisi ya Geneva ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) alisema kwenye mahojiano na Redio ya UM ya kwamba shirika linakabiliwa na upungufu wa dola milioni 46 zinazohitajika kidharura kununua tani 33,000 za chakula ili kuhudumia umma ulioathirika na mapigano katika jimbo la Kivu Kasakazini. Alisema tangu mwezi Agosti watu 200,000 walilazimika kuhama makazi katika sehemeu za mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa sababu ya kufufuka tena kwa mapigano baina ya majeshi ya Serikali na makundi ya waasi. Kadhalika matatizo ya utapiamlo yameanza kushuhudiwa miongoni mwa watoto wa eneo hilo.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu (UNFPA), ambalo ni mwanachama wa Kundi la Uhamaji Duniani (GMG), limewasilisha ripoti ya pamoja yenye kutilia mkazo wajibu wa Mataifa kuhifadhi haki za kimsingi za wahamaji. Ripoti ilionya ya kuwa utovu wa kuhishimu haki za wahamaji ni kitendo kinachowapunguzia uwezo wa kuchangisha juhudi zao katika ukuzaji wa maendeleo ya mataifa waliohamia. Kwa hivyo, ripoti imependekeza kwa mataifa husika, yote mawili – yaani mataifa walipotokea na walipofikia wahamiaji – kuchukua hatua zinazofaa kipamoja kuhakikisha haki za wahamiaji zinalindwa na kuridhiwa kisheria.

KM wa UM Ban Ki-moon pamoja na Robert Zoellick Ijumaa alasiri walitiliana sahihi makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa jumla pakijiri hali ya mtafaruku, uhasama na maafa ya kimaumbile na katika kipindi baada ya mizozo hiyo kudhibitiwa. Makubaliano haya yamekusudiwa hasa kuongoza ushirikiano wao kwa kiasi ambacho kitaridhisha na kusaidia kihakika kuitatua mizozo na maafa ya kimaumbile yenye kuathiri mataifa mara kwa mara.