Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 63

Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 63

Jamii ya kimataifa inaiadhimisha siku ya leo, kote ulimwenguni, kuwa ni “Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Umoja wa Mataifa” ambapo miaka 63 iliopita, mnamo tarehe 24 Oktoba 1945 UM ulianzishwa rasmi.

”Huu ni mwaka muhimu sana kwenye maisha ya UM. Hivi karibuni tumeshakamilisha nusu ya ule muda uliopendekezwa kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) – yenye mtazamo wa kilimwengu katika ujenzi wa dunia ilio bora kwenye karne ya ishirini na moja. Tumetambua kihakika kwenye sherehe za mwaka huu za kuadhimisha Sikuu Kuu ya UM kwamba nchi nyingi bado zimezorota kwenye juhudi zao za kuyatekeleza, kwa wakati, yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia, kabla ya kufikia 2015. Vile vile nina wasiwasi mkubwa juu ya athari za jumla za mzozo wa fedha duniani katika utekelezaji wa Malengo haya ya Milenia. Hakuna wakati ambao ninaamini kutahitajika uongozi bora, na uhusiano wa kipamoja wa kimataifa, kuyatekeleza malengo haya, kama kipindi cha sasa hivi. Ushirikiano miongoni mwa Mataifa Wanachama ndio njia busara iliobakia ya kufuatwa kuleta mafanikio ya kuridhisha katika siku za baadaye. Tizama namna ushirikiano wa kimataifa ulivyosaidia kuwasilisha maendeleo katika kutibu malaria – juhudi hizi za pamoja zimetuwezesha kukaribia kuleta mafanikio ya kudumu kuudhibiti ugonjwa hatari wa malaria, maradhi ambayo kila nukta 30 huua mtoto. Mafanikio haya yamepatikana kwa sababu ya kuwepo sera bora za kitaifa, msaada wa fedha maridhawa wa kutoka wahisani wa kimataifa, usimamizi bia miongoni nchi wanachama na mchango wa utaalamu wa kisayansi na kiteknolojia wa hadhi ya juu kabisa kukabiliana na malaria."