Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUC imeripoti kuzuka tatizo gumu la kiutu katika JKK kufuatia mapigano mapya

MONUC imeripoti kuzuka tatizo gumu la kiutu katika JKK kufuatia mapigano mapya

Shirika la UM linalohusika na Ulinzi wa Amani katika Jamhuriya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) limeripoti kwamba ofisi zake kwenye mji wa Goma, katika eneo la mashariki, zilihujumiwa na mamia ya waandamanaji walioshtumu UM umeshindwa kuwapatia hifadhi na ulinzi unofaa dhidi ya mashambulio ya waasi wa kundi la CNDP linaloongozwa na Jenerali Mtoro Laurent Nkunda.

Ilivyokuwa hali inazidi kuharibika kwenye sehemu za mashariki, katika JKK, Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) imeripoti kuingiwa wasiwasi juu ya taratibu za kuchukuliwa kidharura kudhibiti bora mahitaji ya kiutu, kwa umma uliong’olewa makazi kwa sababu ya mapigano, umma ambao idadi yao, tangu mwezi Agosti, inakadiriwa kufikia 250,000. Umma huu vile vile utahitaji kugawana misaada ya kiutu ya kimataifa na wahamiaji wa ndani wengine 850,000 wailosajiliwa kuwepo kwenye makazi ya muda Kivu Kaskazini kabla ya mapigano kufukua majuzi. Umma wote huo unategemea misaada ya kihali kutoka wahisani wa kimataifa ili kunusuru maisha, na unahitajia kufadhiliwa haraka msaada wa chakula, makazi ya muda, maji na huduma za usafi pamoja na huduma za afya ya msingi na ulinzi bora, halkadhalika.

KM Ban Ki-moon ametoa taarifa ilioshtumu vikali mashambulio ya waasi wa CNDP dhidi ya walinzi amani wa UM wa MONUC. Vile vile KM amelaumu uhasama uliozuka baina ya waasi na vikosi vya taifa vya JKK, tukio ambalo alisema limekiuka mapatano yao ya kusitisha mapigano. Kutokana na sababu hizo ndipo KM ameiomba Serikali, pamoja na wenye madaraka katika jimbo husika, kuchukua kila hatua inayotakikana ili kuhakikisha utulivu unarejeshewa raia waathiriwa haraka iwezekanavyo, na kuwahimiza washirikiane, kwa ukaribu zaidi, na MONUC ili kukidhi kidharura mahitaji ya raia. KM alisisitiza kwamba MONUC, kwa upande wake, itachukua hatua zote zinazolingana na madaraka iliodhaminiwa nayo na Baraza la Usalama, kuwalinda raia pamoja na mali ya UM kwenye eneo la uhasama. Alisema MONUC pia itatekeleza majukumu yake kisheria ya kuhami watumishi wa UM na majengo yao. Aliyataka makundi yanayopigana kusitisha haraka vurugu lao na kuyataka yajitahidi kusuluhisha matatizo yanayowafarakanisha, yaliokwamisha mipango ya amani ya Nairobi na Goma, kwa utaratibu unaojumlisha majadiliano badala ya mapigano.

Taarifa nyengine juu ya shughuli za ulinzi amani Kongo, imetangazwa leo na Msemaji wa KM, Michele Montas, ya kwamba Liuteni Jenerali Vicente Diaz de Villegas wa Uspeni, aliyeteuliwa karibuni kuwa Kamanda Mkuu wa vikosi vya MONUC, ametangaza, kwa kulingana na sababu za binafsi, ya kuwa hatoweza tena kuendelea na kazi na kuongoza vikosi vya MONUC. Brigadia Jenerali Ishmeel Ben Quartey wa Ghana ameteuliwa kushika, kwa muda, nafasi ya Kaimu Kamnda Mkuu wa majeshi ya MONUC mpaka kamanda mpya atakapochaguliwa tena na KM.