Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya wahamiaji katika JKK inasailiwa na UNHCR

Hali ya wahamiaji katika JKK inasailiwa na UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba ofisi zake ziliopo Goma, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) sasa zinajiandaa kuhudumia misaada ya kihali kwa makumi elfu ya watu waliolazimika kuhajiri vijiji na kambi za wahamiaji wa ndani, kwa sababu ya kuzuka mapigano baina ya waasi na vikosi vya serikali katika eneo la kaskazini.

"Watumishi wa UNHCR waliopo Goma wamo mbioni kutayarisha makazi ya muda kwa watu karibu 30,000 waliolazimika kuhama vijiji na kambi za makazi ya muda, kaskazini ya mji, kwa sababu ya kushadidi kwa mapigano makali baina ya makundi ya waasi na vikosi vya Serikali.” Alisema leo asubuhi timu ya UNHCR, chini ya ulinzi na uangalizi mkubwa wa wanajeshi wa amani, ilielekea kwenye kambi ya Kibati, kilomita 10 kaskazini ya mji wa Goma, kutayarisha mapokezi ya watu wanaokadiriwa 30,000 watakaohitajia kuhudumiwa kihali, kidharura, na UM ili kuwanusuru kimaisha. Kuna vituo viwili, tayari, katika eneo hilo vinavyokutana na UM kuhudumia kihali wahamiaji wa ndani 15,000. Vile vile makumi elfu ya watu wanaoeleka kusini sasa hivi kunusuru maisha wanajumlisha wahamiaji 20,000 waliotokea kambi ya Kibumba, kilomita 30 kaskazini ya Goma, pamoja na watu 10,000 wengine waliowasili kutoka maeneo jirani. Msemaji wa UNHCR alibashiria wahamiaji zaidi watamiminikia kwenye vituo vinavyosimamiwa na UM kutokea eneo la kaskazini kutafuta hifadhi na misaada ya kiutu, kwa sababu ya kutanda kwa vurugu na mapigano kwenye maeneo yao katika siku za karibuni.