Hapa na Pale
John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu ametoa mwito maalumu kwa Serikali, raia na makundi yote ya wanamgambo katika Goma, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuchukua hatua zenye nguvu kamili ya kisheria, kuhami raia waathiriwa na kurahisisha kazi za mashirika yanayohusika na huduma za kiutu kwenye eneo la mgogoro la mashariki.~~
Baraza la Usalama limetangaza taarifa maalumu kwa waandishi habari kuhusu mashambulio ya kujitolea mhanga yaliotukia Ijumatano asubuhi, tarehe 29 Oktoba 2008, kwenye miji ya Hargeisa na Bosasso, Usomali Kaskazini na kusababisha mauaji na majeruhi kadha. Taarifa ya Baraza la Usalama ililaani vitendo hivyo, vilivyotafsiriwa vya kuchukiza ambavyo vinaaminiwa viliratibiwa kutukia sawia kwenye majengo ya Shirika la um juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP), ofisi ya serikali ya Ethiopia na ofisi za serikali mwenyeji. Baraza limepeleka mkono wa pole kwa waathiriwa wa mashambulio kwa aila zao, na kwa umma na wenye madaraka Usomali na Ethiopia. Wakati huo huowajumbe wa Baraza la Usalama wamewapongeza watumishi wa UM kwa mchango wao wa kuusaidia umma wa Usomali kujiendeleza kimaisha. Taarifa ya Baraza pia imetilia mkazo ulazima wa kuwashika wakosaji walioandaa, na kufadhilia kihali na mali, vitendo karaha vya kigaidi hivyo, na imeyataka Mataifa yote Wanachama, kushirikiana kipamoja, kwa vitendo na wenye madaraka Usomali, kwa kulingana na majukumu ya sheria ya kimataifa yaliojumuishwa kwenye maazimio 1373 (2001) na 1624 (2005).
Raisi wa Baraza Kuu wa UM, Miguel D’Escoto alipohutubia kikao cha kuanzishwa rasmi tume maalumu ya kuzingatia utaratibu mpya wa kuleta mageuzi ili kudhibiti vyema zaidi mfumo wa fedha kimataifa, alisisitiza ulazima wa kurekibisha kimsingi mfumo huo ili kufufua tena hali ya kuaminiana baada ya kuselelea kwa muda mrefu kwenye soko la kimataifa tabia ya ulafi na ulanguzi, hali ambayo anaamini ndio iliochochea mzozo wa uchumi wa kimataifa uliofumka hivi sasa. Tume maalumu hiyo itaongozwa na John Stiglitz, mshindi wa Zawadi ya Nobel kwa Uchumi ya 2001. Kwa mujibu wa Raisi wa Baraza Kuu D’Escoto mfumo wa fedha uliopo duniani kwa sasa hauwakilishi fungamano halisi za uchumi wa kimataifa. Aliwakumbusha wawakilishi wa Mataifa Wanachama katika UM ya kwamba suluhu ya mzozo wa fedha ulimwenguni haitoweza kudumishwa, wala haitoridhisha, mpaka pale nchi zote zitafanya maamuzi kwa utaratibu wa kidemokrasia utakaojumuisha mchango wa nchi zote.