Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa ziada za huduma za kihali za UM katika Goma

Taarifa ziada za huduma za kihali za UM katika Goma

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetupatia taarifa mpya kuhusu juhudi za UM katika ugawaji wa misaada ya kihali katika Goma na maeneo jirani, hususan kwa wale wahamiaji muhitaji walioathirika na mapigano yaliozuka karibuni baina ya vikosi vya Serikali na makundi ya waasi wa CNDP.

Vile vile WFP imeiruhusu UNHCR kutumia ghala zake ziliopo Kibati, kaskazini ya Goma, kuzigeuza makazi ya muda kwa baadhi ya halaiki ya wahamiaji 45,000 waliokusanyika kwenye eneo hilo. WFP imeripoti kuwa ilifanikiwa kugawa misaada ya vyakula vya wiki mbili katika Masisi na Rutshuru, kwa wahamiaji wapya wa ndani waliong’olewa makwao katika mwezi Oktoba, kabla ya mapigano kushadidi na kukwamisha huduma hizo. Kadhalika, WFP imearifu kwamba tangu mwanzo wa Oktoba hadi sasa bado haijafanikiwa kugawa misaada ya chakula katika Nyanzale, jimbo muhimu la mabonde liliopo wilaya ya Rutshuru, magharibi ya Bustani ya Taifa ya Virunga, ambapo tumearifiwa wamekusanyika idadi kubwa ya watu waliopoteza makazi kutokana na mapigano.