Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM alipokuwa New Delhi, Bara Hindi Ijumaa aliwaambia waandishi habari kama katika siku mbili ziliopita alifanikiwa kufanya mazungumzo ya hali ya juu, ya ushauri juu ya hali katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), na Raisi Paul Kagame wa Rwanda, Raisi Joseph Kabila wa JKK na Raisi Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa UMwa Afrika. Kadhalika KM alisema alizungumza na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni wa Marekani, Condoleeza Rice,

Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, Alan Doss amezuru Goma Ijumaa kufanya tathmini ya hali halisi kwenye eneo la mapigano, ambapo pia alikutana na watawala wenyeji na watumishi wanaohudumia misaada ya kiutu kqwenye eneo hilo. Doss alikuwa miongoni mwa ujumbe wa vyeo vya juu uliojumlisha Naibu Waziri wa Nchi za Kigeni wa Marekani juu ya Masuala ya Afrika, Jendayi Frazer, na Ali Bongo Mjumbe wa Umoja wa Afrika kwa JKK. Kwa mujibu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) hali Goma kwa leo ni shwari, na hakuna mapigano mapya yalioripotiwa katika saa 24 zilizopita. Inavyoonyesha ahadi ya kusimamisha mapigano inahishimiwa. Kadhalika inaripotiwa vikosi vya Serikali ya JKK vimerejea kwenye uwanja wa ndege, kutekeleza majukumu ya ulinzi na kuimarisha usalama. Jana usiku vikosi vya MONUC vilifanya doria nzito ya mitaa ya Goma kuwahakikishia raia usalama, hali ambayo ilisitisha vitendo vya wizi na matumizi ya nguvu.

Takwimu za UM zimethibitisha idadi ya vifo katika siku mbili zilizopita, kutokana na utumiaji wa risasi ilikuwa 21, ikijumlisha wanajeshi 8 wa serikali waliopigwa risasi wakati walipokuwa wakiiba na watu kadha walijeruhiwa, halkadhalika.

Kitengo kinachohusika na Haki za Binadamu cha MONUC kimeripoti watumishi wake wanachunguza taarifa walizopokea juu ya matukio kadha ya kunajisi wanawake katika Goma.

UM umetangaza kuna vituo 16 vya UNHCR katika Kivu Kaskazini vinavyowapatia hifadhi watu 100,000, pamoja na kambi za muda 40 zenye kuwapatia makazi ya muda makumi elfu ya raia. Jumla ya wahamiaji hawa wa dharura ndani ya nchi katika Kivu Kaskazini inakiuka miloni moja.

Ijumaa ya leo ni siku ya mwisho ya Uraisi wa Uchina katika Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba. Kuanzia Ijumamosi, tarehe mosi Novemba, Costa Rica itashika Uraisi wa Baraza la Usalama. Balozi Jorge Urbina wa Costa Rica ataripoti wiki ijayo juu ya ajenda ya kazi za Baraza la Usalama kwa mwezi Novemba.