Mkutano wa DPI/NGO Paris unazingatia mchango wa makundi ya kiraia kuimarisha haki za binadamu

Mkutano wa DPI/NGO Paris unazingatia mchango wa makundi ya kiraia kuimarisha haki za binadamu

Kikao cha 61, cha kila mwaka, kilichoandaliwa shirika na Idara ya Habari ya UM (DPI) na mashirika yasio ya kiserikali (NGOs) kimefunguliwa rasmi hii leo kwenye Makao Makuu ya Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mjini Paris, Ufaransa. Hii ni mara ya kwanza mkutano huu kufabnyika nje ya Makao Makuu ya UM.

Azma hasa ya mkutano huu ni kuzingatia taratibu zilizo imara za kuchukuliwa na jumuiya za kiraia, zikishirikiana na wadau wengineo husika, katika kutekeleza haki za binadamu ulimwenguni, kwa viwango vya kimataifa, kikanda, kitaifa na vile vile viwango vya kienyeji. Mkutano wa Paris umewakusanyisha wawakilishi 2,000 ziada wa mashirika yasio ya kiserikali kutoka karibu nchi 90. Mji wa Paris ulichaguliwa kufanyisha mkutano huu kwa sababu hapo ndipo Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu lilipotiwa sahihi katika 1948. Mada ya mkutano wa mwaka huu, au kauli mbiu ya mkutano, inasema "Twathibitisha Haki za Binadamu: Kwa Kuadhimisha Miaka 60 ya Azimio la Kimataifa."

Ujumbe wa KM uliowasilishwa mkutanoni kwa njia ya vidio, ulikumbusha ya kwamba uhuru wa wanadamu na haki za binadamu ni mambo ya haki ambayo watu wingi duniani wamekosa uwezo wa kuyafikia. Alisema ni wajibu wetu sote kuhakikisha haki hizi zinakamilishiwa umma wa kimataifa. Aliongeza kusema kuwa yeye binafsi yupo tayari kufanya kila awezalo kuhakikisha Mwito wa Kimataifa wa kutekeleza haki za binadamu unakidhiwa na kukamilishwa kihakika kwa kila mtu ulimwenguni.